Mazingira FM

Afisa kilimo asiye na shamba la mfano Mara kukiona

23 October 2026, 2:08 am

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi katikati akiwa anapata maelezo kutoka kwa mtaalamu kwenye kilele kongamano la 11 la kilimo misitu

Maafisa kilimo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutumia mashamba ya JKT Rwamkoma kama mashamba darasa yao.

Na Adelinus Banenwa

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi, amewaelekeza maafisa kilimo wote mkoani humo kuanzisha na kuwa na mashamba darasa ya mfano yatakayowawezesha wakulima kujifunza mbinu bora za kilimo na kuimarisha uzalishaji.

Aidha, amewaelekeza maafisa kilimo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutumia mashamba ya JKT Rwamkoma kama mashamba darasa yao, huku akiwataka maafisa misitu kuhakikisha wanakuwa na maeneo yenye misitu kwa ajili ya kuhamasisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi katikati akiwa ameambatana na kiongozi kutoka VI Agroforestry kulia na kushoto ni mkuu wa wilaya ya Musoma kwenye kilele kongamano la 11 la kilimo misitu

Brigedia Jenerali Mtambi ametoa maelekezo hayo wakati wa kuhitimisha Kongamano la 11 la Maonesho ya Kilimo Misitu 2026, lililolenga kuimarisha sekta ya kilimo misitu na kuongeza ushiriki wa makundi mbalimbali katika mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.

Sauti ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Mtambi

Awali, mwakilishi wa vijana, Alon, amesema kuwa kongamano hilo limefikia maazimio mbalimbali yenye lengo la kuwawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa kilimo misitu, kwa kuzingatia kaulimbiu ya mwaka huu inayohimiza ushiriki wa vijana katika sekta hiyo.

Amesema miongoni mwa maazimio yaliyofikiwa ni kuimarisha sera zinazowezesha ushiriki wa vijana katika maamuzi, kuwekeza katika ujuzi na maarifa, kuboresha huduma za ugani pamoja na kuwezesha upatikanaji wa ardhi na maeneo ya uwekezaji.

Maazimio mengine yanalenga kuondoa vikwazo vinavyowakabili vijana ili waweze kutumia fursa zilizopo katika sekta ya kilimo misitu kwa maendeleo yao na ya taifa kwa ujumla.

Sauti ya Alon