Mazingira FM

Mara waja na “rudi nyumbani jenga nyumbani,”

12 October 2026, 12:08 pm

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Ndugu Kambarage Masubo akizungumza na wakazi wa mara kuhusu kampeni ya “Rudi Nyumbani Jenga Nyumbani,”

“Kampeni hii imeanzishwa kutokana na baadhi ya wazawa wa Mara kuondoka katika mkoa huu na kwenda kutafuta fursa za kiuchumi katika maeneo mengine, ambako wamekuwa wakijenga nyumba nzuri, kuanzisha biashara na kuwekeza katika shughuli mbalimbali, huku maeneo yao ya asili yakibaki bila uwekezaji“

Na Ally Nyamkinda

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Ndugu Kambarage Masubo, amesema jumuiya hiyo imeanzisha kampeni maalumu inayolenga kuwahamasisha wazaliwa wa Mkoa wa Mara wanaoishi nje ya mkoa huo kurejea nyumbani na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Akizungumza kuhusu kampeni hiyo, Ndugu Masubo amesema imepewa jina la “Rudi Nyumbani Jenga Nyumbani,” ikiwa na lengo la kuwahamasisha wanaMara walioko katika mikoa mbalimbali nchini na maeneo mengine kurejea katika maeneo yao ya asili na kuelekeza sehemu ya mitaji na uwekezaji wao katika kukuza uchumi wa mkoa huo.

Amesema kampeni hiyo imeanzishwa kutokana na hali ambayo imekuwa ikijitokeza kwa baadhi ya wazawa wa Mara kuondoka katika mkoa huo na kwenda kutafuta fursa za kiuchumi katika maeneo mengine, ambako wamekuwa wakijenga nyumba nzuri, kuanzisha biashara na kuwekeza katika shughuli mbalimbali, huku maeneo yao ya asili yakibaki bila uwekezaji unaolingana na uwezo wao.

Kwa mujibu wa Ndugu Masubo, hali hiyo imeonesha umuhimu wa kuwa na mpango maalumu utakaowakutanisha wanaMara na kuwahamasisha kutambua nafasi waliyonayo katika kuchangia maendeleo ya mkoa wao, badala ya kuelekeza nguvu na rasilimali zao katika maeneo wanayoishi pekee.

Amesisitiza kuwa kupitia kampeni ya “Rudi Nyumbani Jenga Nyumbani,” jumuiya hiyo inalenga kujenga mwamko miongoni mwa wanaMara ili waweze kuona umuhimu wa kurejea nyumbani, kuwekeza katika biashara, ujenzi wa makazi, kilimo na shughuli nyingine za uzalishaji zitakazochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Sauti ya Kambarage Masubo