Mazingira FM

Viongozi wa kuchaguliwa Mara waanza kupinga ukatili wa keketaji

16 November 2026, 3:43 pm

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Edward Gowele

Miongoni mwa viongozi waliojitokeza katika mapambano hayo ni Diwani wa Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Bugomba Rashidi, ambaye amewataka wanajamii, hususan wazee wa kimila, kuachana na mila ya ukeketaji.

Na Adelinus Banenwa

Ushiriki wa viongozi wa kuchaguliwa katika mapambano dhidi ya mila na desturi zenye madhara kwa jamii, hususan ukeketaji wa watoto wa kike, umeanza kuimarika mkoani Mara kufuatia juhudi za utoaji wa elimu zinazofanywa na serikali pamoja na mashirika yanayotetea haki za wanawake na watoto.

Awali, kutoshiriki kikamilifu kwa baadhi ya viongozi wa kuchaguliwa katika kukemea vitendo hivyo kulitajwa kuwa miongoni mwa changamoto zilizokuwa zikikwamisha juhudi za kupambana na ukatili huo. Hata hivyo, hali imeanza kubadilika ambapo viongozi hao wameanza kujitokeza hadharani kuhamasisha jamii kuachana na vitendo vya ukeketaji.

Diwani wa Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Bugomba Rashidi

Miongoni mwa viongozi waliojitokeza katika mapambano hayo ni Diwani wa Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Bugomba Rashidi, ambaye amewataka wanajamii, hususan wazee wa kimila, kuachana na mila ya ukeketaji akieleza kuwa ina madhara kwa watoto wa kike wanaofanyiwa vitendo hivyo.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Kemambo wilayani Tarime, Bugomba Rashidi

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Edward Gowele, ambaye pia amesisitiza umuhimu wa jamii kukomesha vitendo vya ukeketaji pamoja na tohara zisizo salama, akieleza kuwa kumekuwa na mabadiliko katika mwitikio wa jamii ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Mabadiliko hayo yanatajwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali na wadau mbalimbali katika kuhakikisha jamii inakomesha mila na desturi zenye madhara na kulinda haki, afya na usalama wa wanawake na watoto.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Edward Gowele