Mazingira FM
Mazingira FM
11 November 2026, 9:41 pm

Awataka wananchi na viongozi wa Wilaya ya Tarime kutoa taarifa za vitendo vya ukeketaji mapema ili hatua stahiki zichukuliwe kuwanusuru watoto wa kike dhidi ya mila hiyo
.Na Edward Lucas.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Wakili Amon Mpanju, amewataka wananchi na viongozi wa Wilaya ya Tarime kutoa taarifa za vitendo vya ukeketaji mapema ili hatua stahiki zichukuliwe kuwanusuru watoto wa kike dhidi ya mila hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha waathirika wanapata huduma kwa wakati.
Mpanju ameyasema hayo Novemba 10, 2026, wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukeketaji uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Sekondari Bukira, Wilaya ya Tarime mkoani Mara, akibainisha kuwa ushiriki wa wananchi katika kutoa taarifa na kushirikiana na vyombo husika ni muhimu katika kufanikisha azma ya serikali ya kutokomeza ukeketaji.
Amesema pamoja na jitihada za elimu zinazoendelea nchini, Mkoa wa Mara bado unakabiliwa na kiwango kikubwa cha ukeketaji, ambapo kwa mujibu wa Utafiti wa Afya ya Uzazi na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022, asilimia 28 ya wanawake na watoto wa kike katika takwimu zilizotajwa wamekeketwa, hali inayoufanya mkoa huo kuwa miongoni mwa mikoa mitatu inayoongoza kwa vitendo hivyo nchini, licha ya wastani wa kitaifa kushuka kutoka asilimia 10 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 8 mwaka 2022.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Tarime wamepongeza kampeni hiyo na kuitaka serikali kuifanya endelevu, wakisema ushiriki wa viongozi wa ngazi za juu kutoka wizarani unaongeza nguvu katika kuhamasisha wazazi na vijana kushiriki mapambano dhidi ya ukeketaji, huku wakisisitiza kuwa jukumu hilo linapaswa kubebwa na jamii nzima.

