Mazingira FM

Watoto wa kike 53 waokolewa dhidi ya ukeketaji Mara

14 November 2026, 12:15 am

Mtaalamu kutoka idara ya maendeleo ya jamii

Katika ziara hiyo, timu hiyo imefanikiwa kufikia kata tisa na vijiji 18 katika halmashauri hizo tatu, ambapo jumla ya watu 17,000 wamepatiwa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji

Na Adelinus Banenwa

Timu ya kutoa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, kwa kushirikiana na wataalamu wa maendeleo ya jamii wa Mkoa wa Mara na halmashauri za Serengeti, Rorya na Tarime, imehitimisha ziara yake ya kuelimisha jamii kuhusu madhara ya vitendo vya ukeketaji.

Katika ziara hiyo, timu hiyo imefanikiwa kufikia kata tisa na vijiji 18 katika halmashauri hizo tatu, ambapo jumla ya watu 17,000 wamepatiwa elimu kuhusu madhara ya ukeketaji na umuhimu wa kulinda haki na usalama wa watoto wa kike.

Baadhi ya wananchi waliojitokeza katika kampeni ya kupinga ukeketaji

Mafanikio mengine ya ziara hiyo ni kuokolewa kwa watoto wa kike 53 ambao walikuwa katika hatari ya kukeketwa na wazazi wao, hatua inayotajwa kuwa mchango muhimu katika mapambano dhidi ya mila hiyo yenye madhara.

Ziara hiyo imelenga kuongeza uelewa wa jamii, kuhamasisha wazazi na walezi kuachana na vitendo vya ukeketaji pamoja na kuimarisha ulinzi wa watoto wa kike katika jamii.

Sauti ya mtaalamu kutoka idara ya maendeleo ya jamii