Mazingira FM
Mazingira FM
8 September 2026, 8:39 pm

Walifanikiwa kupata usafiri na kumpeleka katika Hospitali ya Manyamanyama kwa ajili ya matibabu, lakini licha ya juhudi za madaktari, Daudi alifariki dunia kutokana na kupoteza damu nyingi zilizotokana na majeraha aliyoyapata.
Na Adelinus Banenwa
Mwendesha pikipiki maarufu wa bodaboda, aliyetambulika kwa jina la Daudi Komanya (24), mkazi wa Kisangwa wilayani Bunda, anadaiwa kuuawa na watu wasiojulikana baada ya kushambuliwa na watu hao, ambao kisha waliondoka na pikipiki yake.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mtaa wa Mugaja, Kata ya Manyamanyama, Sani Marko Ngeleja, tukio hilo limetokea majira ya saa moja na nusu usiku wa kuamkia leo, Septemba 8, 2026, katika eneo la Mugaja Shule ya Msingi.
Ngereja amesema kuwa waliposikia kelele katika eneo hilo, walikwenda kufuatilia na kumkuta Daudi akiwa anavuja damu nyingi. Kijana huyo aliwaeleza kuwa ameshambuliwa na kunyang’anywa pikipiki yake, huku akiwaomba msaada wa kufikishwa hospitalini.
Amesema walifanikiwa kupata usafiri na kumpeleka katika Hospitali ya Manyamanyama kwa ajili ya matibabu, lakini licha ya juhudi za madaktari, Daudi alifariki dunia kutokana na kupoteza damu nyingi zilizotokana na majeraha aliyoyapata.
Kwa upande wake, Michael Rubale, ambaye ni mmoja wa madereva wa bodaboda wanaokaa na Daudi katika kituo kimoja cha Romani, Bunda, ameiambia Mazingira FM kuwa jana walikuwa pamoja na Daudi katika kituo hicho hadi majira ya jioni, lakini baadaye hawakujua alielekea wapi.
Michael amesema walipata taarifa kuhusu tukio hilo baada ya dereva aliyekuwa amempa Daudi pikipiki kufika kituoni na kuwajulisha kuwa Daudi ameshambuliwa na yupo hospitalini akiwa katika hali mbaya.
Amesema baadhi ya madereva bodaboda walikwenda hospitalini kumjulia hali mwenzao, huku wengine wakianza kufuatilia maeneo mbalimbali kwa lengo la kumbaini na kumkamata mtu anayehusishwa na tukio hilo.
Hata hivyo, jitihada hizo hazikuzaa matunda, na majira ya saa tatu usiku Daudi alifariki dunia. huku waliokuwa wakifuatilia mtuhumiwa walirejea bila mafanikio ya kumkamata.
Michael ameiomba Serikali kupitia Jeshi la Polisi kuongeza juhudi za kumtafuta na kumkamata mtuhumiwa au wahusika wa tukio hilo, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.
Jitihada za kuwatafuta jeshi la polisi zinaendelea ili kutoa taarifa zaidi kuhusiana na tukio hili