Mazingira FM

Wananchi watakiwa kutoa ushahidi wa ukatili wa kijinsia

23 August 2026, 8:44 pm

Afisa wa Jeshi la Polisi kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Bunda, Renata Ramadhani, Picha na Edward Lucas

Wananchi wanapaswa kutambua kuwa kutoa ushahidi wa tukio la ukatili wa kijinsia ni sehemu ya kumsaidia mwathirika kupata haki

Na. Edward Lucas

Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya sheria kwa kutoa ushahidi wa matukio ya ukatili wa kijinsia wanapohitajika, ili kusaidia waathirika kupata haki zao kisheria.

Wito huo umetolewa na Afisa wa Jeshi la Polisi kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Bunda, Renata Ramadhani, wakati akizungumza katika kipindi cha Mwanga wa Jamii kinachorushwa na Radio Mazingira FM, kilichojadili mada isemayo “Ukatili wa Kijinsia Unaripotiwaje, kutoka tukio linapotokea hadi mwathirika kupata haki.”

Afande Renata amesema ushahidi ni muhimu katika hatua za kisheria dhidi ya watuhumiwa wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo jamii inapaswa kushirikiana na vyombo vya sheria kwa kutoa ushahidi inapohitajika.

Amesema wananchi wanapaswa kutambua kuwa kutoa ushahidi wa tukio la ukatili wa kijinsia ni sehemu ya kumsaidia mwathirika kupata haki, akisisitiza kuwa mtu anayekataa kumsaidia mwenzake leo, anaweza kukutana na hali kama hiyo yeye mwenyewe au mwanafamilia wake siku nyingine.

Afisa wa Jeshi la Polisi kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Bunda, Afande Renata Ramadhani. Picha na Edawrd Lucas
Sauti ya Afande Renata Ramadhani

Akieleza utaratibu wa kuripoti tukio hadi mwathirika kupata haki, Renata amesema hatua ya kwanza ni kutoa taarifa mapema katika eneo linaloweza kushughulikia tukio hilo kwa haraka, ikiwemo kituo cha polisi kilicho karibu, ofisi za serikali za mitaa au mtu anayeaminika na anayeweza kusaidia kufikisha taarifa kwa mamlaka husika.

Amesema baada ya taarifa kutolewa, mwathirika na mashahidi wanapaswa kuwa tayari kushirikiana na vyombo vya sheria kwa kutoa taarifa na ushahidi unaohitajika ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa dhidi ya mtuhumiwa.

Sauti ya Afande Renata Ramadhan

Kwa upande wao, baadhi ya wasikilizaji walioshiriki mjadala huo wamepongeza elimu waliyoipata, huku wengine wakihoji pia nafasi ya wanaume katika kupata msaada na haki pale wanapofanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Sauti za wasikilizaji wakichangia mada