Mazingira FM

Mshikamano katika ndoa husaidia wanawake kiuchumi

9 August 2026, 7:25 am

Rebecca Shilinde mwalimu mstaafu na mjasiriamali wa mapambo na bidhaa za urembo, mkazi wa Nyashimo mkoani Simiyu katika maonesho ya nanenane eneo la Nyakabindi

Rebecca anaeleza kuwa shughuli zake za ujasiriamali zimemsaidia kuchangia mahitaji ya nyumbani, mahitaji ya wanafunzi na kuboresha makazi ya familia.

Na Edward Lucas

Ushirikiano, uaminifu na kusaidiana kati ya wanandoa umetajwa kuwa miongoni mwa misingi inayoweza kumsaidia mwanamke kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kuchangia maendeleo ya familia, huku pia ukisaidia kupunguza migogoro ndani ya familia.

Hayo yameelezwa na Rebecca Shilinde, mwalimu mstaafu na mjasiriamali wa mapambo na bidhaa za urembo, mkazi wa Nyashimo mkoani Simiyu, wakati wa mahojiano yaliyofanyika katika viwanja vya maonesho ya Nanenane Nyakabindi mkoani Simiyu, ambako alikuwa akionesha na kutangaza bidhaa zake.

Rebecca, ambaye aliamua kutumia kwa vitendo ujuzi wa stadi za kazi aliokuwa akifundisha shuleni baada ya kustaafu, anasema safari yake ya ujasiriamali imekuwa na mchango mkubwa kutoka kwa mume wake, ambaye amekuwa akimpa taarifa za fursa, kumsaidia katika mahitaji ya biashara na kumpa nafasi ya kushiriki katika maonesho na maeneo mbalimbali ya kutafuta fursa.

Sauti ya Rebecca Shilinde mwalimu mstaafu
Eneo la maonesho nanenane nyakabindi mkoani Simiyu

Rebecca anasema ushirikiano huo unahitaji pia uaminifu kutoka kwa pande zote, akieleza kuwa nafasi na msaada anaopewa mwanamke katika shughuli za kiuchumi vinapaswa kuambatana na uwajibikaji na kujikita katika malengo yaliyokusudiwa.

Rebecca anaeleza kuwa shughuli zake za ujasiriamali zimemsaidia kuchangia mahitaji ya nyumbani, mahitaji ya wanafunzi na kuboresha makazi ya familia, huku maonesho ya Nanenane yakiwa miongoni mwa fursa zinazomsaidia kukutana na wateja, kutangaza bidhaa na kujifunza fursa nyingine za biashara.

Sauti ya Rebecca Shilinde mwalimu mstaafu

Akizungumza na wanawake wengine wanaojishughulisha na biashara, Rebecca amewataka kutumia fursa za mafunzo yanayotolewa na taasisi mbalimbali ili kuongeza maarifa na ujuzi wa biashara na ujasiriamali.