Mazingira FM
Mazingira FM
20 June 2026, 6:02 pm

Amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa wabunifu katika kuandaa miradi yenye tija itakayoinua vipato vya wananchi badala ya kuendelea kuipa kipaumbele mikopo ya bodaboda pekee.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evance Alfred Mtambi, amezitaka halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha zinatoa kwa wakati mikopo ya asilimia 10 inayotengwa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kiuchumi.
Maagizo hayo ameyatoa Juni 19, 2026, wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha uwasilishaji wa taarifa ya utekelezaji wa hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Kanali Mtambi amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii kuwa wabunifu katika kuandaa miradi yenye tija itakayoinua vipato vya wananchi badala ya kuendelea kuipa kipaumbele mikopo ya bodaboda pekee. Amesema ni muhimu kuanzisha miradi mingine ikiwemo ufugaji wa samaki, ufyatuliaji wa matofali pamoja na kilimo cha bustani za mboga mboga.

Aidha, Kanali Mtambi amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, George Mbilinyi, kuhakikisha wataalamu wa halmashauri hiyo wanatoa elimu kwa wananchi kuhusu shughuli za uzalishaji mali ili kuongeza vipato vyao. Amesema baadhi ya wananchi wanaoishi katika maeneo ya fukwe bado wanajishughulisha na shughuli zisizo na tija kwa maendeleo yao.
Mkuu huyo wa Mkoa ameelekeza zaidi ya shilingi milioni 316 za miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zielekezwe katika ujenzi wa miundombinu ya nishati safi ya kupikia ili kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Katika hatua nyingine, Kanali Mtambi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kwa kupata hati safi ya ukaguzi. Amesema mafanikio hayo yanaonesha halmashauri hiyo imeanza vizuri katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.
Aidha, amesisitiza Baraza la Madiwani kuendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mpango kazi utakaohakikisha maagizo yote ya Kamati za Bunge pamoja na hoja zilizobaki za ukaguzi zinafanyiwa kazi kikamilifu.