Mazingira FM
Mazingira FM
5 July 2026, 2:06 pm

Ni wajibu wa kila mwandishi kuhakikisha kuwa kompyuta, simu, na mitandao yao inalindwa kwa njia salama wakati wote.
Na Adelinus Banenwa
Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) umewataka waandishi wa habari nchini kuacha tabia ya kujisahau na badala yake kipaumbele chao cha kwanza kielekezwe katika kulinda usalama wa afya zao za akili, miili yao, pamoja na ulinzi wa mifumo yao ya kidijitali wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.
Rai hiyo imetolewa mkoani Morogoro na mwakilishi kutoka UTPC, Edmund Kipungu, wakati wa ufungaji wa mafunzo maalum ya siku tatu yaliyolenga kuwajengea uwezo wanahabari.
Mafunzo hayo yamehusisha jumla ya waandishi wa habari 12 waliochaguliwa kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara pamoja na Zanzibar.
Akifafanua malengo ya mafunzo hayo, Kipungu amesema kuwa UTPC imeona kuna uhitaji mkubwa wa kuwasaidia waandishi wa habari kutambua vihatarishi na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza kazini. Amesema hatua hiyo itawasaidia kuchukua tahadhari mapema na kujua mbinu sahihi za kuepukana na hatari hizo kabla hazijaleta madhara makubwa kwao na kwa vyombo vyao vya habari.

Katika hatua nyingine, mkufunzi wa mafunzo hayo na mtaalamu wa ulinzi wa mifumo ya kidijitali, Bushiri Ulaya, ameeleza namna eneo la usalama wa mtandao linavyopuuzwa na baadhi ya wanahabari. Ulaya ametahadharisha kuwa uzembe huo unawaweka waandishi katika hatari kubwa ya kudukuliwa kwa taarifa zao binafsi, akaunti zao, pamoja na siri za vyanzo vyao vya habari.
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa kila mwandishi kuhakikisha kuwa kompyuta, simu, na mitandao yao inalindwa kwa njia salama wakati wote.

Moja washiriki wa mafunzo hayo kutoka mkoani Morogoro Shukuru Materu ameshukuru kupata fursa hiyo, akieleza kuwa elimu hiyo imekuwa na tija kubwa na imewazindua. amekiri kuwa kwa muda mrefu waandishi wa habari wamekuwa wakipigania usalama na haki za watu wengine katika jamii, huku wao wenyewe wakijisahau na kujiweka kwenye mazingira hatarishi.
Akihitimisha mafunzo hayo, Mkurugenzi wa UTPC amebainisha kuwa mkakati huo ni sehemu ya malengo ya muda mrefu ya taasisi hiyo kuleta mabadiliko ya kiusalama na kupunguza vihatarishi vinavyowakabili wanahabari uwandani.

Mkurugenzi huyo ametoa wito kwa washiriki hao 12 kuwa mabalozi wema kwa kuisambaza elimu hiyo kwa waandishi wenzao waliopo kwenye vituo vya kazi na klabu zao za waandishi ili malengo yaliyokusudiwa na taasisi hiyo yaweze kutimia kote nchini.