Mazingira FM
Mazingira FM
4 July 2026, 1:03 am

Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mguu wa kulia pamoja na baadhi ya viungo vingine vya mwili vilikuwa vimeondolewa.
Na Adelinus Banenwa
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linaendelea na uchunguzi wa kifo cha mtoto Simon Juma Bango (11), mkazi wa Nyasura Makumbusho, Wilaya ya Bunda, ambaye mwili wake ulipatikana ukiwa umeanza kuharibika huku baadhi ya viungo vya mwili vikiwa vimeondolewa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Pius Lutumo, amesema mtoto huyo alikuwa mwanafunzi wa Darasa la Tano katika Shule ya Msingi Mazoezi.
Kwa mujibu wa Kamanda Lutumo, Juni 24, 2026, Simon aliondoka nyumbani kwenda kufanya biashara ya kuuza maandazi, lakini hakurejea nyumbani, jambo lililoifanya familia yake kuanza juhudi za kumtafuta.
Baada ya juhudi hizo kutofanikiwa, familia ilitoa taarifa katika Kituo cha Polisi, ambapo Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wananchi lilianzisha msako wa kumtafuta.
Mwili wa mtoto huyo ulipatikana katika kichaka kilichopo eneo la Chuo cha Ualimu Bunda, ukiwa umeanza kuharibika.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mguu wa kulia pamoja na baadhi ya viungo vingine vya mwili vilikuwa vimeondolewa.
Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi ili kubaini waliohusika na tukio hilo na kuwachukulia hatua za kisheria.