Mazingira FM

DC Kaminyoge aongoza mazishi ya diwani Ruth Irungu

12 June 2026, 10:27 am

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Aswege Enock Kaminyoge, akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Ruth Hosea Irungu

Marehemu Mheshimiwa Ruth Hosea Irungu alifariki dunia Juni 5, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, mkoani Mwanza, alipokuwa akipatiwa matibabu.

Na Adelinus Banenwa

Aliyekuwa Diwani wa Viti Maalum wa Kata ya Iramba, Wilaya ya Bunda mkoani Mara, Marehemu Mheshimiwa Ruth Hosea Irungu, amezikwa 11 Juni 2026 katika Kijiji cha Isanju, Kata ya Iramba, huku mamia ya waombolezaji, viongozi wa serikali, wanasiasa na wananchi wakijitokeza kutoa heshima zao za mwisho.

Shughuli za mazishi ziliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Aswege Enock Kaminyoge, ambaye aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani, utulivu, usalama na upendo ili kuifanya Bunda kuwa wilaya ya mfano wa kuigwa.

Mheshimiwa Kaminyoge pia amewasisitiza watumishi wa serikali kuhakikisha wananchi wanaofika katika ofisi mbalimbali wanapatiwa huduma stahiki na changamoto zao kutatuliwa kwa wakati bila kujali ukubwa wa tatizo husika.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Mheshimiwa Kangi Lugola, amesema kifo cha Marehemu Ruth Hosea Irungu ni pigo kubwa kwa wananchi na viongozi wa jimbo hilo, akieleza kuwa amepoteza mjumbe muhimu wa Kamati ya Mfuko wa Jimbo ambaye alikuwa mchapakazi, mwadilifu na mkarimu.

Mbunge wa Jimbo la Mwibara, Mheshimiwa Kangi Lugola

Mheshimiwa Lugola ameieleza familia ya marehemu kuendelea kuyaenzi na kuyaishi mema yote aliyoyaacha wakati wa uhai wake, akisisitiza kuwa mchango wake katika maendeleo ya wananchi utaendelea kukumbukwa kwa vizazi vijavyo.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, Ndugu George Mbilinyi, amesema kifo hicho kimemnyima mshauri muhimu aliyekuwa akitoa ushauri na kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya halmashauri hiyo.

Waheshimiwa madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Bunda wakitoa heshima zao za mwisho kwa diwani mwenzao Ruth Hosea

Aidha, amewashukuru Waheshimiwa Madiwani pamoja na watumishi wa Halmashauri kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha katika kipindi chote cha maombolezo hadi kufanikisha shughuli za mazishi ya marehemu.

Marehemu Mheshimiwa Ruth Hosea Irungu alifariki dunia Juni 5, 2026 katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando, mkoani Mwanza, alipokuwa akipatiwa matibabu. Enzi za uhai wake alitambulika kama kiongozi mwenye maono, mchapakazi na aliyekuwa mstari wa mbele katika kusimamia na kuhamasisha shughuli za maendeleo kwa wananchi wa Kata ya Iramba na Wilaya ya Bunda kwa ujumla.