Mazingira FM

Maoni mseto ugawaji vyandarua Saranga Bunda

13 August 2026, 6:04 am

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Saranga Bunda wakisubiri kupatiwa Chandarua

Jumla ya kaya 670 zinatarajiwa kunufaika na vyandarua katika mtaa wa Saranga.

Na Adelinus Banenwa

Zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa wananchi kwa lengo la kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria linaendelea katika maeneo mbalimbali ndani ya Wilaya ya Bunda, huku wananchi wa Mtaa wa Saranga mjini Bunda wakitoa maoni tofauti kuhusu zoezi hilo.

Baadhi ya wananchi waliopata vyandarua wamepongeza hatua ya Serikali kuwapatia vyandarua bure, wakisema vitawasaidia kujikinga na kung’atwa na mbu wakati wa usiku na hivyo kupunguza hatari ya kupata malaria licha ya vyandarua hivyo kutolewa vichache.

Sauti za baadhi ya wananchi waliopata vyandarua

Hata hivyo, baadhi ya wananchi ambao hawakufanikiwa kupata vyandarua wamelalamikia utaratibu wa uandikishaji, wakisema waandikishaji walipita mara moja tu, hivyo mtu ambaye hakuwa nyumbani siku hiyo amekosa fursa ya kupata chandarua.

Wananchi hao wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kuwapatia vyandarua wale ambao hawakuandikishwa ili nao waweze kujikinga na malaria.

Sauti za baadhi ya wananchi walikosa vyandarua
Mwenyekiti wa Mtaa wa Saranga, Philipo Safari

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Saranga, Philipo Safari, amesema zoezi la ugawaji wa vyandarua linaendelea vizuri na linatarajiwa kukamilika ndani ya siku tatu, huku akisema mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa.

Mwenyekiti Safari amesema jumla ya kaya 670 zinatarajiwa kunufaika na vyandarua katika mtaa huo.

Mwenyekiti Safari amesema majina ya wananchi ambao hawakuandikishwa tayari yamekusanywa na yatafikishwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kupata maelekezo, huku akisisitiza kuwa kwa sasa vyandarua vinatolewa kwa wale walioandikishwa.

Baadhi ya wakazi wa mtaa wa Saranga Bunda wakisubiri kupatiwa Chandarua
Sauti ya Philipo Safari

Zoezi hilo linaendelea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Bunda, likiwa na lengo la kuongeza matumizi ya vyandarua na kusaidia kupunguza maambukizi ya malaria.