Mazingira FM

Butiama: Mila zinavyowakosesha wanawake haki ya kumiliki mali

27 September 2026, 6:42 pm

“ukosefu wa elimu ya kisheria, hofu na mfumo dume kuwa miongoni mwa changamoto zinazowafanya baadhi ya wanawake kushindwa kudai haki zao”

Na Edward Lucas.

Mila na desturi za baadhi ya koo zinazoweka mwanamke nyuma katika urithi wa mali zimetajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia wanawake katika Wilaya ya Butiama kukosa fursa ya kumiliki ardhi na mali nyingine za familia.

Diwani Mstaafu wa Kata ya Butiama, Richard Mkonazi Kiganga, anasema zamani katika jamii hiyo mwanamke hakuwa na nafasi ya kuzungumzia masuala ya mali au ardhi, huku maamuzi mengi yakifanywa na baba wa familia.

Sauti ya Richard Mkonazi Kiganga

Kiganga anaeleza kuwa hali hiyo ilijidhihirisha pia wakati wa kifo cha baba wa familia, ambapo mali na ardhi zingeweza kuchukuliwa na ndugu wa kiume, huku wanawake na watoto wa familia wakiachwa bila mamlaka juu ya mali hiyo.

Sauti ya Richard Mkonazi Kiganga

Afisa wa Dawati la Msaada wa Kisheria Butiama, Grayson Martine, anasema hali hiyo imeendelea kuchangia migogoro ya umiliki wa ardhi, akitaja ukosefu wa elimu ya kisheria, hofu na mfumo dume kuwa miongoni mwa changamoto zinazowafanya baadhi ya wanawake kushindwa kudai haki zao.

Sauti ya Grayson Martine

Hata hivyo, Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Butiama, Veronica Wanzita Lucas, anasema hali imeanza kubadilika kutokana na elimu ya sheria na uwepo wa vyombo vya utatuzi wa migogoro, huku wanawake wengi wakionyesha ujasiri zaidi wa kudai haki zao za mali na ardhi.

Sauti ya Veronica Wanzita Lucas

Wadau hao wanasisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu ya sheria kuhusu mirathi, wosia na haki ya kumiliki mali, ili mila na desturi zisije zikawa kikwazo cha wanawake na watoto wa kike kupata haki zao katika familia.