Mazingira FM

Hofu ya kupoteza kura isikwamishe mapambano dhidi ya ukeketaji-Mara

25 November 2026, 8:52 pm

Kulwa Lazaro, Afisa Miradi wa Catholic Sister’s Network

viongozi wa kisiasa watakiwa kutumia nafasi zao kuelimisha jamii na kupinga ukeketaji badala ya kuogopa kupoteza uungwaji mkono wa kisiasa katika uchaguzi kutoka kwa jamii zinazounga mkono mila hiyo.

.Na Edward Lucas.

Viongozi wa kisiasa wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya vitendo vya ukeketaji kwa kutanguliza usalama na haki za mtoto wa kike badala ya kuogopa kupoteza uungwaji mkono wa kisiasa kutoka kwa jamii zinazounga mkono mila hiyo.

Wito huo umetolewa na Afisa Miradi wa The Catholic Sisters Network Against Gender-Based Violence in Tanzania. (CSN-AGBV), Kulwa Lazaro, akisema viongozi hao wana nafasi muhimu katika kuleta mabadiliko ya kimtazamo na kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoathiri watoto wa kike, hususan katika Mkoa wa Mara.

Akizungumza na Radio Mazingira FM, Lazaro amesema viongozi wanapaswa kutumia nafasi zao kuelimisha jamii na kupinga mila na desturi zinazohatarisha maisha na mustakabali wa watoto wa kike, bila kuathiriwa na hofu ya masuala ya kisiasa na uchaguzi.

Sauti ya Kulwa Lazaro

Amesema juhudi za kupambana na ukeketaji zinahitaji ushirikiano wa viongozi wa kisiasa, Serikali na wadau wengine ili kuhakikisha jamii inaachana na vitendo hivyo na kulinda haki za watoto.

Kwa upande wake, Catholic Sisters Network imefanikiwa kuwafikia wanafunzi 3,500 katika shule 56 mkoani Mara kwa mwaka wa 2025/2026 kupitia elimu kuhusu ukatili wa kijinsia, hususan ukeketaji.

Sauti ya Kulwa Lazaro