Mazingira FM
Mazingira FM
15 October 2026, 8:55 pm

Bado kuna changamoto ya unyanyapaa na kuwafungia ndani watu wasioona, hali inayowanyima fursa za elimu na huduma zingine za kijamii.
Na Edward Lucas.
Chama cha Wasioona Tanzania (TLB) kimeitaka jamii kuondoa unyanyapaa na mitazamo hasi dhidi ya watu wasioona, kikisisitiza kuwa kutokuona hakumaanishi kukosa uwezo, vipaji wala mwelekeo wa maisha.
Wito huo umetolewa leo, Oktoba 15, 2026, katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Fimbo Nyeupe yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mlobezi, Lamadi, wilayani Busega, mkoani Simiyu, yenye kaulimbiu isemayo “Kutoona Sio Kupoteza Dira.”
Katika risala ya TLB, Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Loata Lomitu Molel, amesema bado kuna changamoto ya unyanyapaa na kuwafungia ndani watu wasioona, hali inayowanyima fursa za elimu na huduma nyingine za kijamii.

Molel amesema pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali na wadau, bado kuna haja ya kuboresha shule na huduma za kijamii ili ziwe rafiki na fikivu kwa watu wasioona. Ameongeza kuwa TLB ina wajibu wa kuendelea kufanya utetezi na ushawishi, huku akiomba wadau kuunga mkono juhudi za chama hicho katika kuwawezesha wanachama kiuchumi na kuimarisha rasilimali za chama.
Maadhimisho hayo yametanguliwa na kongamano la siku mbili lililoanza Oktoba 13, likiwakutanisha wanachama takribani 250 kutoka mikoa 22 ya Tanzania Bara, kwa ajili ya kujifunza na kujadili mikakati ya kuwawezesha watu wenye ulemavu wa kuona. Katika kilele hicho, TLB pia imegawa fimbo nyeupe kwa ajili ya watu wasioona kupitia wawakilishi kutoka maeneo mbalimbali.
Kwa upande wake, mgeni rasmi na Mwenyekiti wa TLB Taifa, Habiba Salum Ngulangwa, amewahimiza watu wasioona kutokata tamaa, bali kujituma na kutumia fursa za mafunzo ya ujasiriamali ili kujenga maisha ya kujitegemea.

Ngulangwa amesema kutokuona hakupaswi kuwa sababu ya mtu kujitenga na jamii, akisisitiza umuhimu wa kuchangamkia fursa zilizopo ili kujitegemea na kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Maadhimisho hayo yanaweka msisitizo juu ya wajibu wa jamii kuhakikisha watu wasioona wanapata haki, huduma na fursa sawa, kwa kuzingatia kaulimbiu isemayo: Kutoona Sio Kupoteza Dira.