Mazingira FM

Wanafunzi 271 kuhitimu Migungani Sec, changamoto za shule zatajwa

7 October 2026, 7:36 pm

Baadhi ya wanafunzi wahitimu kidato cha nne migungani Sec 2026

Miongoni mwa changamoto ni upungufu wa walimu, vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta, pamoja na ukosefu wa maabara kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kupata elimu ya vitendo.

Na Adelinus Banenwa

Jumla ya wanafunzi 271, wakiwemo wasichana 139 na wavulana 132, wanatarajiwa kuhitimu Kidato cha Nne katika Shule ya Sekondari Migungani, iliyopo wilayani Bunda.

Hayo yameelezwa leo, Oktoba 7, 2026, wakati wa mahafali ya tatu ya shule hiyo, ambapo kupitia risala ya wanafunzi pamoja na taarifa ya shule iliyowasilishwa na Mkuu wa Shule, Mwalimu Boaz Elias, imeelezwa kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Mkuu wa Shule, Mwalimu Boaz Elias

Changamoto hizo ni pamoja na ujenzi wa jiko la kupikia chakula cha wanafunzi ambao umefikia hatua ya boma, uhitaji wa matundu 28 ya vyoo, mabweni ya wanafunzi, pamoja na nyumba za walimu, ambapo shule haina hata nyumba moja.

Changamoto nyingine ni upungufu wa walimu, vifaa vya TEHAMA ikiwemo kompyuta, pamoja na ukosefu wa maabara kwa ajili ya kuwawezesha wanafunzi kupata elimu ya vitendo.

Risala ya wanafunzi
Sauti ya Mkuu wa Shule, Mwalimu Boaz Elias taarifa ya shule
Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Bunda, Mwalimu James Mnyeti Gambuna

Akijibu risala ya wanafunzi na taarifa ya shule kwa niaba ya Mbunge wa Bunda Mjini, Mhe. Esther Bulaya, ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Chama cha Walimu Wilaya ya Bunda, Mwalimu James Mnyeti Gambuna, amesema Mhe. Bulaya ameahidi kutoa mashine ya kurudufu mitihani, maarufu kama photocopy, pamoja na kompyuta moja.

Mwalimu Mnyeti amesema vifaa hivyo vitasaidia kupunguza changamoto ya uchapishaji wa mitihani shuleni, huku akieleza kuwa mgeni rasmi ameahidi pia kushirikiana na wadau wengine katika kutafuta suluhisho la changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo

Sauti ya Mwalimu James Mnyeti Gambuna