Mazingira FM

Wazazi watakiwa kupinga ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike

13 October 2026, 11:09 am

Warioba Juma Warioba, Afisa Ustawi wa Jamii halamashauri ya mji wa Bunda akiwa studio za Radio Mazingira Fm

Baadhi ya jamii bado zinaendeleza mila na desturi zinazochangia kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo

.Na Edward Lucas.

Wazazi na walezi wametakiwa kushiriki kikamilifu katika programu mbalimbali za malezi, ulinzi na ustawi wa watoto ili kuwakinga dhidi ya vitendo vya ukatili, ikiwemo kunyimwa haki ya elimu, mimba za utotoni na ndoa za utotoni.

Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, mkoani Mara, Warioba Juma Warioba, wakati akizungumza katika kipindi cha Duru za Habari kinachorushwa na Radio Mazingira FM, kilichojadili masuala ya ulinzi na maendeleo ya mtoto wa kike katika Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike.

Warioba amesema baadhi ya wazazi wamekuwa wakisahau wajibu wao katika kusimamia malezi na makuzi ya watoto, ikiwemo kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu, usalama na ulinzi wanapokuwa nyumbani na nje ya nyumbani.

Sauti ya Warioba Juma Warioba

Akizungumzia changamoto ya ndoa za utotoni, Warioba amesema baadhi ya jamii bado zinaendeleza mila na desturi zinazochangia kuwaozesha watoto wa kike wakiwa na umri mdogo. Amesema hali hiyo inachochewa na baadhi ya wazazi wanaotanguliza manufaa ya mali au matarajio mengine kuliko haki, usalama na mustakabali wa watoto wao.

Ameeleza kuwa vitendo hivyo vinakiuka haki za mtoto wa kike na vinaweza kumnyima fursa ya kupata elimu na kutimiza ndoto zake.

Sauti ya Warioba Juma Warioba

Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike huadhimishwa kila mwaka Oktoba 11 kwa lengo la kuhamasisha ulinzi wa haki za wasichana na kuangazia changamoto zinazowakabili duniani, zikiwemo ndoa za utotoni, ukatili na vikwazo vya kupata elimu.

Nchini Tanzania, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imetangaza kaulimbiu isemayo “Wekeza kwa Mtoto wa Kike: Tokomeza Ndoa za Utotoni.”

Kaulimbiu hiyo inahimiza wazazi, walezi, viongozi na jamii kwa ujumla kuwekeza katika elimu, afya, usalama na ustawi wa mtoto wa kike, huku wakichukua hatua za kupinga mila na desturi zinazokiuka haki zake.