Mazingira FM

Marufuku kukatisha Lamadi kwenda Bunda kwa miguu au baiskeli

28 September 2026, 8:56 pm

Mkuu wa Wilaya hiyo, Aswege Enock Kaminyoge

Zaidi ya asilimia 99.7 ya wakazi wa Nyatwali wamelipwa fidia yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 52.

Na Adelinus Banenwa

Serikali wilayani Bunda mkoani Mara, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Aswege Enock Kaminyoge, imekabidhi rasmi eneo lililokuwa Kata ya Nyatwali kwa Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), kwa ajili ya kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Aswege Enock Kaminyoge, amesema zaidi ya asilimia 99.7 ya wakazi wa Nyatwali wamelipwa fidia yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 52.

Baadhi ya maafisa na askali katika zoezi la kukabidhi eneo la iliyokuwa kata ya nyatwali kwa TANAPA

Hata hivyo, amesema bado kuna maeneo ambayo baadhi ya wananchi wanaendelea kuwasilisha malalamiko kuhusu fidia, likiwemo eneo la Magwata, Mjapani na Masanga, akisisitiza kuwa serikali itaendelea kuyashughulikia na wananchi wenye haki watalipwa.

DC Aswege ameiagiza TANAPA kuhakikisha hakuna mtu anayeingia katika eneo hilo bila kibali kutoka kwa Kamishna wa Uhifadhi. Aidha, amesema kuanzia sasa wananchi hawaruhusiwi kutumia barabara inayotoka Lamadi kwenda Bunda kwa kutembea kwa miguu au kutumia baiskeli.

Sauti ya Aswege Enock Kaminyoge
Ismail Omari, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti

Kwa upande wake, Ismail Omari, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, kwa niaba ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Magharibi, Godwell Ole Menglateki, amesema wamepokea maelekezo ya serikali na wako tayari kuyafanyia kazi, huku akiwataka wananchi kuzingatia sheria za uhifadhi.

Sauti ya Ismail Omari, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti