Mazingira FM

ECO SAFE yatoa mafunzo na vifaa kinga kwa wakusanya taka Bunda

23 November 2026, 10:05 am

Kwenye picha ya pamoja kati ya wanufaika wa mafunzi ya ECO SAFE Organisation na wawezeshaji

Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wakusanya taka uelewa kuhusu umuhimu wa mchango wao katika kutunza mazingira, pamoja na kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi.

Na Adelinus Banenwa

Shirika la Eco Safe limetoa mafunzo kwa wakusanya taka zaidi ya 40 kutoka Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa lengo la kuimarisha afya na usalama mahali pa kazi, pamoja na kuwajengea uwezo wa kutambua na kujikinga na vihatarishi wanavyokutana navyo wakati wa kutekeleza majukumu yao. Mafunzo hayo yameambatana na utoaji wa vifaa kinga ili kuhakikisha wakusanya taka wanafanya kazi katika mazingira salama.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa wa Mkoa wa Mara, Erick Muhigi, amewataka wataalamu wa halmashauri kuendelea kuwajengea uwezo wakusanya taka, huku akiwatahadharisha kuwa makini na taka zenye kemikali, zilizooza na vipande vya chupa vinavyoweza kusababisha majeraha na magonjwa. Aidha, ameipongeza Eco Safe kwa kutoa vifaa kinga na kuwataka wanufaika kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa badala ya kuviuza au kuvitumia kwa shughuli nyingine, akisema mpango huo unaweza kuufanya Mji wa Bunda kuwa mfano kwa halmashauri nyingine tisa za Mkoa wa Mara.

Sauti ya Afisa wa Mkoa wa Mara, Erick Muhigi,
Mkurugenzi wa Shirika la Eco Safe, Pendo Manyama akizungumza katika semina ya wakusanya taka Bunda mjini

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Eco Safe, Pendo Manyama, amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea wakusanya taka uelewa kuhusu umuhimu wa mchango wao katika kutunza mazingira, pamoja na kuzingatia afya na usalama mahali pa kazi. Amesema matumizi ya vifaa kinga, maarufu kama PPEs, ni muhimu wakati wote wanapotekeleza majukumu yao, na kwamba wameanza na washiriki 40 kwa kuwapatia elimu na vifaa kinga ili wawe mfano wa kuigwa na wengine.

Sauti ya mkurugenzi wa Shirika la Eco Safe, Pendo Manyama

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Said Ramadhan, amewapongeza wakusanya taka kwa mchango wao katika usafi wa mazingira, lakini akawataka kuzingatia maadili ya kazi na kuepuka vitendo vya uharibifu wa mali za umma na watu binafsi. Amesema hivi karibuni wanafunzi walikamatwa kwa tuhuma za kung’oa madirisha ya chuma katika madarasa mawili ya Shule ya Sekondari Migungani, wakidai kuagizwa na wakusanya vyuma chakavu kwa malipo ya shilingi 3,000, huku akisisitiza kuwa vitendo kama uvunjaji wa makaburi na wizi wa vyuma havipaswi kuvumiliwa.

Sauti ya Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Said Ramadhan
Mmoja ya mkusanya taka akikabidhiwa vifaa kinga kwa lengo la kujilinda wakati akitekeleza majukumu yake ya usafi

Kwa upande wao, baadhi ya wakusanya taka walioshiriki mafunzo hayo wamelishukuru shirika la Eco Safe kwa kuwapatia elimu na vifaa kinga, wakieleza kuwa awali hawakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu vihatarishi vinavyoweza kuathiri afya na usalama wao kazini. Aidha, wametoa wito kwa wakusanya vyuma chakavu wanaojihusisha na wizi wa vifaa vya watu kuacha tabia hiyo, kwa kuwa inachafua taswira ya wengine wanaofanya kazi hiyo kwa uadilifu.

Sauti za baadhi ya wakusanya vyuma chakavu mjni Bunda