Mazingira FM
Mazingira FM
17 September 2026, 9:28 pm

Ni muhimu tahadhari hiyo kuwafikia wananchi mapema ili waweze kuchukua hatua stahiki kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, amewataka madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi kuhusu athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El-Nino.
Mhe. Kaminyoge ametoa agizo hilo wakati akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kilichofanyika katika kikao cha robo ya nne cha mwaka wa fedha 2025/2026.
Amesema ni muhimu tahadhari hiyo kuwafikia wananchi mapema ili waweze kuchukua hatua stahiki kujikinga na madhara yanayoweza kusababishwa na mvua hizo, ikiwemo mafuriko na uharibifu wa miundombinu.
Mkuu huyo wa Wilaya amewataka madiwani kutumia Kamati za Maafa kuanzia ngazi ya Wilaya, Halmashauri, Kata hadi Vijiji, kwa ajili ya kuainisha maeneo yanayoweza kuwa hatarishi wakati wa mvua kubwa.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutambua mapema maeneo salama ambayo wananchi wanaweza kuhamia endapo majanga yatatokea, ili kuzuia madhara kwa maisha na mali.

Kwa upande wao, baadhi ya madiwani wamesema wako tayari kuanza kutoa elimu kwa wananchi katika maeneo yao kuhusu namna ya kuchukua tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Madiwani hao pia wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka katika maeneo yenye changamoto za miundombinu ya barabara, hususan kuzibua mitaro na kuondoa uchafu kwenye makaravati, ili kurahisisha upitishaji wa maji na kupunguza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko.
Baadhi ya wananchi wa Bunda wamesema tayari wamepata taarifa kuhusu uwezekano wa mvua hizo kupitia vyombo mbalimbali vya habari pamoja na mitandao ya kijamii, na wameanza kuchukua tahadhari mbalimbali.
Wananchi hao wamesema miongoni mwa hatua wanazochukua ni kufanya usafi katika maeneo yao ya makazi na mazingira yanayowazunguka, huku wakitoa wito kwa jamii kuendelea kuchukua tahadhari ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
Wameongeza kuwa pamoja na kuchukua hatua za kujikinga, wanaendelea kumuomba Mungu ili mvua hizo zisilete madhara makubwa, ikiwemo milipuko ya magonjwa ambayo inaweza kujitokeza kutokana na changamoto za mazingira na maji.