Mazingira FM

Walimu sita mbaroni kifo cha mwanafunzi Bunda

20 August 2026, 9:27 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo

Hadi sasa walimu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi, huku uchunguzi wa kitabibu ukisubiriwa ili kubaini chanzo halisi cha kifo.

Na Adelinus Banenwa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amethibitisha kifo cha mwanafunzi Peter Maira, aliyekuwa mwanafunzi wa Kidato cha Sita katika Shule ya Sekondari Makongoro, iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Kamanda Lutumo amesema mwanafunzi huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, baada ya kudaiwa kuzimia wakati akipewa adhabu shuleni.

Kwa mujibu wa Kamanda Lutumo, hadi sasa walimu sita wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi, huku uchunguzi wa kitabibu ukisubiriwa ili kubaini chanzo halisi cha kifo cha mwanafunzi huyo.

Kamanda Lutumo ameeleza kuwa wakati mwanafunzi huyo akipewa adhabu, alizirai na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu, lakini baadaye alipoteza maisha.

Sauti ya Kamanda Pius Lutumo

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, amewataka wanafunzi pamoja na wazazi kuendelea kuwa watulivu na kusubiri matokeo ya uchunguzi unaoendelea, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kufuatilia suala hilo kwa mujibu wa sheria.

Aidha, Kamanda Lutumo amesema suala la aina na utaratibu wa adhabu zinazotolewa shuleni linapaswa kuachwa kwa taasisi husika ya elimu, ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuratibu na kusimamia taratibu za utoaji wa adhabu katika shule.

Sauti ya Kamanda Pius Lutumo

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini mazingira yaliyopelekea kifo cha mwanafunzi Peter Maira.