Mazingira FM

Wadau wapendekeza fursa za kiuchumi kwa mangariba kuzuia ukeketaji Tarime

28 September 2026, 5:41 pm

Baadhi ya wadau waliojitokeza kujadili mipango na mikakati kuwasaidia manusura wanaokimbia ukeketaji mkoani Mara

“Kutoa fursa mbadala za kiuchumi kwa mangariba kunaweza kusaidia kupunguza sababu za ukeketaji”

Na Edward Lucas.

Wadau wa kupinga ukeketaji wilayani Tarime mkoani Mara wamependekeza kuwezeshwa kwa wazee wa kimila na mangariba kama sehemu ya mikakati ya kuzuia ukeketaji wa watoto wa kike, kwa kuzingatia nafasi yao katika jamii na baadhi yao kunufaika kiuchumi kupitia mila hiyo.

Pendekezo hilo limetolewa katika kikao kilichoandaliwa na Safe Society Platform Tanzania (Jukwaa la Kijamii), kilichowakutanisha viongozi wa serikali, jeshi la polisi, ustawi wa jamii na mashirika binafsi kujadili mikakati ya kuwalinda watoto wa kike wanaokabiliwa na ukeketaji na maandalizi ya kambi salama kwa watoto watakaoukimbia.

Afisa Ustawi wa Jamii Tarime, Fatna Maneno amesema kutoa fursa mbadala za kiuchumi kwa mangariba kunaweza kusaidia kupunguza sababu inayowafanya baadhi yao kuendelea kuhusika katika vitendo vya ukeketaji, sambamba na elimu kwa jamii kuhusu madhara yake kwa mtoto wa kike.

Sauti ya Fatna Maneno

Kwa upande mwingine, wadau wamesema juhudi za kukomesha ukeketaji zinahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, mashirika na jamii, huku elimu ikitolewa kwa wazazi, watoto na viongozi wa kimila ili kubadili mitazamo inayochochea vitendo hivyo. Mwenyekiti Safe Society Platform Tanzania (Jukwaa la Jamii Salama )’, Jacob Sira Matiko, amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuwalinda watoto wa kike hasa wakati wa msimu ambao baadhi ya koo huendesha ukeketaji.

Sauti ya Jacob Siro Matiko, Mwenyekiti wa Safe Society Platform Tanzania
Meja Edward Gowele, Mkuu wa Wilaya ya Tarime (aliyekaa katikati amevaa suti nyeusi) na kulia kwake ni Jacob Sira Matiko, Mwenyekiti wa Safe Society Platform (Jukwaa la Jamii Salama) wakiwa katika kikao na kujadili mikakati ya kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo vya ukeketaji

Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema pamoja na kuendelea kutoa elimu katika shule, nyumba za ibada na jamii, ni muhimu kuwashirikisha wazee wa mila katika juhudi za kukomesha ukeketaji na kuhakikisha watoto wanaokimbia vitendo hivyo wanapata mahali salama pa kukaa badala ya kutegemea maeneo ya muda.

Sauti ya Meja Edward Gowele