Mazingira FM
Mazingira FM
10 November 2026, 10:13 pm

Tukio hilo linatokea wiki tatu tu tangu mvua nyingine iliyoambatana na upepo mkali iliposababisha nyumba 301 kuezuliwa katika kata hiyo, huku nyumba 31 zikianguka kabisa.
Na Adelinus Banenwa
Mvua iliyokuwa imeambatana na upepo mkali imeezua paa la chumba kimoja cha darasa katika Shule ya Msingi Nyasana, iliyopo Kata ya Kabasa, Halmashauri ya Mji wa Bunda, pamoja na nyumba moja katika Mtaa wa Kalisumba.
Akizungumza na Mazingira FM, Diwani wa Kata ya Kabasa, Mhe. Daniel Yona Magembe, amesema mvua hiyo ilidumu kwa takribani dakika 10 pekee, lakini iliambatana na upepo mkali uliosababisha uharibifu huo.
Aidha, Kamati ya Usalama pamoja na Kamati ya Maafa, zikiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, zimefika katika eneo la tukio katika Shule ya Msingi Nyasana kwa ajili ya kufanya tathmini ya athari zilizosababishwa na mvua hiyo.

Mhe. Magembe amesema tukio hilo linatokea wiki tatu tu tangu mvua nyingine iliyoambatana na upepo mkali iliposababisha nyumba 301 kuezuliwa katika kata hiyo, huku nyumba 31 zikianguka kabisa.
Amesema baadhi ya wananchi walioathirika na maafa hayo ya awali bado wanaendelea kujihifadhi kwa ndugu, jamaa na marafiki kutokana na uharibifu wa makazi yao.
Kutokana na matukio hayo, Mhe. Magembe ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kuzingatia usalama wao mara wanapoona dalili za mvua, hasa zile zinazoambatana na upepo mkali.