Mazingira FM

Dr Mwigulu: kufutwa sheria ya kutaifisha mifugo si ruhusa ya kukiuka sheria

3 October 2026, 7:30 pm

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, akihutubia wananchi wakati wa ziara ya kiongozi huyo wilayani Bunda

Amesisitiza kuwa wananchi wote wana wajibu wa kuendelea kuheshimu sheria na taratibu zilizopo ili kuepusha migogoro.

Na Adelinus Banenwa

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa kufutwa kwa sheria iliyokuwa ikiruhusu kutaifishwa kwa mifugo hakuwapi wafugaji uhuru wa kukiuka sheria na taratibu za ufugaji.

Dk. Mwigulu amesema hatua ya kuifuta sheria hiyo imelenga kuzuia utekelezaji ambao ungeweza kuongeza umaskini kwa wananchi, hivyo wafugaji wanapaswa kuhakikisha mifugo yao haisababishi migogoro na wananchi wengine.

Akizungumza na wananchi mkoani Mara leo, Oktoba 3, 2026, Waziri Mkuu amesema wafugaji hawapaswi kutumia nafasi hiyo kuingiza mifugo katika maeneo yasiyoruhusiwa, yakiwemo hifadhi na mashamba.

Baadhi ya wananchi kwenye mkutano wa waziri mkuu wilayani Bunda

Amesisitiza kuwa wananchi wote wana wajibu wa kuendelea kuheshimu sheria na taratibu zilizopo ili kuepusha migogoro.

Aidha, Dk. Mwigulu amesema kama wananchi wanavyotakiwa kutokujichukulia sheria mkononi, vyombo vya ulinzi na usalama navyo vinapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria.

Baadhi ya wananchi kwenye mkutano wa waziri mkuu wilayani Bunda

Amesema vitendo vya kujichukulia sheria mkononi huacha makovu yasiyopona, hivyo ametoa wito kwa pande zote kuheshimu sheria na kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha migogoro.

Sauti ya waziri mkuu Dk. Mwigulu Nchemba

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza kupatiwa taarifa kuhusu ujenzi wa majengo mawili ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda yaliyoanguka.

Mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Bunda aliyeshika kipaza sauti akitoa maelezo kwa waziri mkuu hospitali ya bunda DC wakati wa ziara ya kiongozi huyo wilayani Bunda

Dk. Mwigulu amesema iwapo taarifa hiyo itathibitisha kuwa kuanguka kwa majengo hayo kulitokana na uzembe uliofanyika kwa makusudi, watumishi waliohusika wanapaswa kuwajibishwa kwa kufukuzwa kazi.

Amesema hatua hiyo inapaswa kuchukuliwa licha ya baadhi ya watumishi hao kuwa wamehamia ndani ya Mkoa wa Mara, akisisitiza kuwa uwepo wa wataalamu katika ujenzi unapaswa kuhakikisha kazi inafanyika kwa kuzingatia viwango na taratibu.

Sauti ya waziri mkuu Dk. Mwigulu Nchemba