Mazingira FM
Mazingira FM
8 November 2026, 10:35 pm

“Kutokana na elimu kutufikia najilaumu kwanini nilikeketwa na nikaruhusu watoto wangu kukeketwa, najilaumu kwanini…”
Na Edward Lucas.
Wananchi wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara wameeleza namna elimu kuhusu madhara ya ukeketaji ilivyobadili mitazamo yao, huku baadhi wakikiri kushiriki katika mila hiyo hapo awali lakini sasa wakipinga na kuamua kuwalinda watoto wa kike dhidi ya vitendo hivyo.
Wakizungumza katika uzinduzi wa kampeni ya kupinga ukeketaji ulioratibiwa na kusimamiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, uliofanyika Novemba 6, 2026, katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kisumwa, wamesema elimu imewafanya kutambua madhara ya ukeketaji na umuhimu wa kuachana na mila zenye madhara.
Mmoja wa wananchi hao amesema awali alikuwa hajui madhara ya ukeketaji na aliwahi kuwakeketa watoto wake watatu wa kike, lakini baada ya kupata elimu aliamua kuzuia watoto wake wengine watatu wasikeketwe huku Mwananchi mwingine aliyewahi kukeketwa amesema anajutia kitendo hicho kilichotokana na kufuata mila, huku akieleza kuwa elimu imewasaidia wananchi kuanza kukataa ukatili wa kijinsia na kuhamasishana kuachana na vitendo hivyo.
Akizungumzia kampeni hiyo, Dennis Mose, Mratibu wa Dawati la Kitaifa la Kutokomeza Vitendo vya Ukeketaji kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, amesema Serikali imeanzisha kampeni hiyo kutokana na kutambua kuwa mwaka 2026 ni kipindi kinachohusishwa na ongezeko la ukeketaji kwa jamii ya Mara, hivyo jitihada maalumu zinafanyika kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi ya vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Anna Mgelwa, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka wizara hiyo, amesema kampeni hiyo inalenga kuelimisha jamii na si kuwakamata wananchi, akisisitiza kuwa ukeketaji ni ukatili wa kijinsia na ni kinyume cha Sheria ya Mtoto, Sura ya 13. Ameeleza kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 163 cha sheria hiyo, mtu atakayebainika kufanya ukeketaji anakabiliwa na adhabu ya faini ya Sh milioni tano hadi 15, pamoja na fidia ya madhara aliyoyapata mtoto.