Mazingira FM

Diwani Machilu; “mkipata semina andaa vikundi fedha za mikopo zipo’

24 June 2026, 3:35 pm

Uundwaji wa vikundi hivyo utarahisisha upatikanaji wa mikopo pamoja na kuongeza ushirikiano miongoni mwa wananchi katika kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo.

Na Adelinus Banenwa

Diwani wa Kata ya Manyamanyama, Mhe. Mathayo Machilu, amewataka wananchi waliojitokeza kushiriki semina ya ujasiriamali kuhakikisha wanafuatilia kwa umakini mafunzo yatakayotolewa ili waweze kupata maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Machilu ametoa rai hiyo wakati akifungua rasmi semina ya siku tatu ya ujasiriamali aliyoandaa kwa wananchi wa kata hiyo na maeneo jirani, ikiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kuanzisha na kuendesha shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa tija.

Amesema mafunzo hayo ni fursa muhimu kwa wananchi kujifunza mbinu za biashara, usimamizi wa miradi na namna ya kutumia fursa zilizopo kujiongezea kipato na kuboresha maisha yao.

baadhi ya washiriki wa semina hiyo

Aidha, baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, Mhe. Machilu amewahimiza washiriki kuunda vikundi vyenye angalau watu watano ili kuwawezesha kunufaika na fursa za mikopo inayotolewa na Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa vikundi vya wananchi.

Amesema uundwaji wa vikundi hivyo utarahisisha upatikanaji wa mikopo pamoja na kuongeza ushirikiano miongoni mwa wananchi katika kuanzisha na kuendeleza miradi ya maendeleo.

Sauti ya diwani wa Kata ya Manyamanyama, Mhe. Mathayo Machilu

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa semina hiyo wamepongeza hatua ya diwani huyo kuandaa mafunzo hayo, wakisema yatawasaidia kupata uelewa mpana wa masuala ya ujasiriamali na kuwafungulia fursa za kujiongezea kipato.

baadhi ya washiriki wa semina hiyo

Semina hiyo ya siku tatu inatarajiwa kuwahusisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Kata ya Manyamanyama na kutoa mafunzo kuhusu ujasiriamali, usimamizi wa fedha, uundaji wa vikundi vya kiuchumi pamoja na namna ya kunufaika na mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri.