Mazingira FM

Bunda yazindua jukwaa la vijana kuimarisha fursa za kiuchumi

30 July 2026, 7:54 pm

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, jukwaa hilo linatarajiwa kuwa daraja la mawasiliano kati ya vijana na Serikali, huku likichochea ushiriki mkubwa wa vijana katika shughuli za maendeleo na uchumi wa eneo hilo.

Na Adelinus Banenwa

Fursa za kiuchumi kwa vijana zimeendelea kusisitizwa baada ya Halmashauri ya Mji wa Bunda kuzindua Jukwaa la Vijana litakalokuwa kiungo cha kuwaunganisha vijana na taarifa za fursa mbalimbali za maendeleo pamoja na kushirikiana na Serikali katika kutatua changamoto zinazowakabili.

Akizindua jukwaa hilo, Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha vijana kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo na kunufaika na fursa zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali.

Sauti ya Aswege Enock Kaminyoge,

Kwa upande wake, afisa maendeleo ya vijana halmashauri ya mji wa Bunda, Maliki Saidi Ndumbwe, amesema jukwaa hilo litatumika kama sauti ya vijana, likiwaunganisha kupitia viongozi waliochaguliwa ili kushirikiana na Serikali katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili. Amesema pamoja na kuhamasisha ujasiriamali na ajira, jukwaa hilo pia litajikita katika kuimarisha maadili na afya ya vijana.

Sauti ya Maliki Saidi Ndumbwe

Nao baadhi ya vijana walioshiriki katika kongamano hilo wamepongeza Serikali kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kuanzisha jukwaa hilo, wakisema litawarahisishia kupata taarifa za fursa na kuwajengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi. Wametoa wito kwa vijana wengine kujitokeza kushiriki katika makongamano na programu za maendeleo ili kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa.

Sauti za baadhi ya vijana

Kwa mujibu wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, jukwaa hilo linatarajiwa kuwa daraja la mawasiliano kati ya vijana na Serikali, huku likichochea ushiriki mkubwa wa vijana katika shughuli za maendeleo na uchumi wa eneo hilo.