Mazingira FM
Mazingira FM
15 May 2026, 1:19 pm

Mkama alieleza kuwa anatambua kazi ya ukunga na uuguzi ni wito wa kujitolea unaoendelea kuwa msaada mkubwa kwa jamii, huku akipongeza ufanisi mkubwa wa kazi hiyo kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani.
Na Adelinus Banenwa
Hospitali ya Wilaya ya Teule ya Bunda (Bunda DDH) imefanya maadhimisho ya Siku ya Wauguzi na Wakunga Duniani tarehe 15 Mei 2026, huku mgeni rasmi Ndugu Wilson Mkama akichangia shilingi milioni nane kwa ajili ya kuboresha huduma za afya hospitalini hapo.
Mchango huo umetolewa wakati wa harambee maalum iliyolenga kutatua changamoto za uhaba wa vifaa tiba kwa watoto njiti na mifumo ya hewa ya oksijeni.
Katika kilele cha maadhimisho hayo yaliyofanyika hospitalini hapo, wataalamu wa afya wametakiwa kuendeleza moyo wa kujitolea na upendo katika kuhudumia wagonjwa, hasa wakizingatia misingi iliyoachwa na mwanzilishi wa uuguzi duniani, Florence Nightingale, katika karne ya 19.

Akizungumza na wahudumu hao, mgeni rasmi Ndugu Mkama alieleza kuwa anatambua kazi ya ukunga na uuguzi ni wito wa kujitolea unaoendelea kuwa msaada mkubwa kwa jamii, huku akipongeza ufanisi mkubwa wa kazi hiyo kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani.

Awali, akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Katibu wa Hospitali ya Bunda DDH, Adelad Mchuruza, amebainisha mafanikio makubwa ya hospitali hiyo katika utoaji wa huduma na kueleza kuwa hospitali hiyo inapokea zaidi ya watoto 300 wanaozaliwa kabla ya kufikisha miezi tisa (Watoto njiti) kila mwaka, ambapo zaidi ya watoto 120 kati yao wanatoka nje ya Halmashauri ya Mji wa Bunda.
Ili kuendelea kuokoa maisha ya watoto hao na kuboresha utoaji huduma, Katibu huyo alitoa wito kwa serikali, wadau, na taasisi mbalimbali kujitokeza kuchangia vifaa tiba zaidi. Alisisitiza kuwa hospitali inakabiliwa na uhaba wa mashine za kulelea watoto njiti na inahitaji haraka kusimikwa kwa mfumo wa kisasa wa kusambaza hewa ya oksijeni wodini badala ya kutumia mitungi ya sasa inayoleta usumbufu katika kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja.