Mlida: Bajeti ya mifugo imeongezeka kutoka bilion 169 hadi 460
7 July 2024, 4:08 pm
Katika kipindi cha miaka mitatu serikali ya awamu ya sita imefanya mengi katika sekta ya mifugo ikiwemo ujenzi wa majosho, kuongeza bajeti ya wizara, ununuzi wa pembejeo za mifugo, uchimbaji wa mabwawa ya mifugo n.k.
Na Adelinus Banenwa
Imeelezwa kuwa serikali imefanya kazi kubwa katika sekta ya mifugo ambapo imepandisha bajeti ya wizara hiyo kutoka shilingi 169 bilioni hadi shilingi 460 bilioni katika kipindi cha miaka mitatu.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa chama cha wafugaji Tanzania na mjumbe wa bodi ya NARCO Ndugu Mlida Mushota alipozungumza na Mazingira Fm ambapo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya serikali ya awamu ya sita upande wa sekta ya mifugo imepata fedha nyingi kutoka serikalini ikiwemo kuboresha miundombinu kwa wafugaji.
Mlida amesema katika kipindi hicho cha miaka mitatu mbali na kuongezeka kwa bajeti ya wizara pia wafugaji wapatao elfu 8,400 wamepata mikopo, pia hekta zipatazo million 3.5 zimepimwa na kumilikishwa kwa wafugaji.
Aidha amesema katika kipindi cha mwaka 2023 na 2024 zimesambazwa lita za dawa za mifugo zipatazo lita elfu 56 zenye thamani ya shilling bilion 2.6, majosho 751 yenye thamani ya shilingi bilion 16.
Sambamba na hilo pia Mlida amesema minada ipatayo 15 ya kisasa imejengwa, pia serikali imechimba mabwawa 20 ya wafugaji hivyo anaamini serikali itaendelea kuithamini sekta ya mifugo huku akiwataka wafugaji kumiliki ardhi maana ndiyo nyenzo kuu ya mfugaji.
Katika hatua nyingine ameyataka mabaraza ya madiwani na halmashauri kutenga na kupima maeneo ya wafugaji pia kuboresha minada badala ya kusubiri kutoza ushuru wa mifugo tu huku hawatengenezi mazingira mazuri kwa wafugaji.