Mazingira FM

Serengeti: Aliwa na Mamba wakati akivuka Mto Mara kwenda Shambani

14 September 2023, 8:02 am

Picha kutoka maktaba ya Radio Mazingira haina uhusiano na tukio hili.

Kufuatia tukio la mwananchi kukamatwa na kuliwa na mamba, Mkuu wa mkoa wa Mara awasisitiza wananchi kutofanya shughuli zao ndani ya hifadhi ya mto Mara

Na Edward Lucas

Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda amewasisitiza wananchi kutofanya shughuli zao ndani ya maeneo ya hifadhi ya mto Mara ili kuepuka madhara yanayojitokeza kwa binadamu na athari za uharibifu wa vyanzo vya maji.

Mtanda ametoa kauli hiyo jana tarehe 13 Septemba 2023 wakati akizindua Maadhimisho ya 12 ya siku ya Mto Mara baada ya kupokea taarifa ya mwananchi wa kijiji cha Nyansurumunti Kata ya Kisaka Wilaya ya Serengeti, Nyambabe William (50) kukamatwa na kuliwa na mamba wakati akivuka mto kwenda shambani kwake.

Awali akitoa taarifa za tukio hilo wakati wa zoezi la upandaji wa miti na uwekaji wa vigingi katika eneo la Mto Mara kijiji cha Borenga, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma amemuomba mkuu wa mkoa kuwasaidia kuwavuna mamba hao

Ayub Mwita Makuruma, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti

Tukio hili limetokea wakati serikali na wadau wengine wa Uhifadhi wa Mazingira wakiwa katika jitihada za kupanda miti na kuweka alama ili kuzuia shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 ya Mto Mara ambapo WWF kwa ufadhili wa USAID wamekusudia kupanda miti 44,000 na kuweka vigingi 50