Mazingira FM

Bunda: Tarura walaumiwa kung’oa vibao vya Anwani za makazi Bila kushirikisha viongozi wa kata kabarimu

15 July 2022, 8:26 pm

Wajumbe wa kikao cha WDC kata ya kabarimu walalamikia uongozi wa Tarura Bunda katika hatua ya kuondoa na kubadilisha majina ya vibao vya barabara katika zoezi la anuani za makazi huku wakidai linapelekea usumbufu mkubwa kwao

Wakizungumza katika kikao kilichofanyika Leo July 15 2022 eneo la shule ya msingi kabarimu katika Halmashauri ya Mji wa Bunda wajumbe hao wamesema zoezi la uwekaji vibao katika mitaa na barabara liliwafanya watumie nguvu kubwa katika kuwachangisha wananchi kama ilivyoelekezwa awali na hivyo kitendo cha Tarura kuviondoa na kubadili majina pasipo kuwashirikisha ni sawa na kuwadharau.

Akichangia hoja hiyo mwenyekiti mtaa wa majengo, Ndugu Mawazo amesema majina yaliyowekwa katika vibao vya anuani za makazi yalitokana na mapendekezo ya wananchi katika vikao vyao na kuchangia fedha ili kuweka vibao hivyo lakini hivi sasa Tarura inaweka vibao vingine vyenye majina tofauti na yaliyopendekezwa na wananchi.

Amesema kitendo cha halmashauri kuagiza wananchi wachangie zoezi la uwekaji wa vibao kwa usimamizi wa viongozi wao kisha Tarura kuanza kuviondoa tena pasipo kuwashirikisha pasipo kujali nguvu, fedha na muda uliotumika ni kuwachonganisha viongozi na wananchi.K

wa upande wake Maseme Masaju aliyemwakilisha mkuu wa shule ya sekondari Nyiendo amesema kitendo cha kuwachangisha wananchi kisha kuelekeza vibao hivyo ving’olewe pasipo kukaa na kuwashirikisha wananchi inapelekea wakati mwingine zoezi la kuwashirikisha wananchi katika shughuli za maendeleo kuwa gumu.

Mwenyekiti mtaa wa Saranga, Philipo Safari amesema kwa upande wake hatoitisha kikao chochote cha mtaa hadi pale ambapo uongozi wa kata au halmashauri utakapofanya kikao na wananchi wa mtaa wake ili kuwapa ufafanuz wa mchakato wa vibao vya anuani za makazi.

Aidha kwa upande mwingine amesema katika mtaa wa Saranga wananchi wamekuwa wakilalamikia uvamizi wa nyani na tumbili katika makazi ya watu na kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

By Edward Lucas