Mazingira FM

ESRF yazinoa radio jamii kuboresha huduma za afya nchini

20 September 2023, 6:52 am

Prof. Fortunata Songora Makene akizungumza na washiriki wa mafunzo. Picha na Edward Lucas

Na Edward Lucas

Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii ESRF Tanzania inaendesha mafunzo kwa waandishi wa habari wa Radio Jamii nchini ili kusaidia katika juhudi za kuboresha huduma za afya katika jamii.

Mafunzo hayo ya siku 4 yameanza leo 19 Septemba 2023 katika ukumbi wa mikutano makao makuu ya taasisi hiyo Jijini Dar es Salaam yakiwashirikisha watangazaji na waandishi wa habari 47 kutoka radio mbalimbali za kijamii.

Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo Mkurugenzi wa ESRF, Prof Fortunata Songora Makene amesema mafunzo hayo yameandaliwa kama sehemu ya mradi wa Utafiti ujulikanao kwa jina la ‘Afya Yako’ ambao umelenga katika tafiti ya maeneo makubwa mawili.

Akiyataja maeneo hayo amesema ni kugundua nafasi ya Redio za jamii katika kupambana na taarifa potofu za afya ya jamii na eneo la pili ni kubaini nafasi ya mwandishi wa habari za uchunguzi katika uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya nchini hususani katika zahanati na vituo vya afya.

Sauti ya Prof. Fortunata Songora Makene
Prof. Fortunata Songora Makene akizungumza na washiriki wa mafunzo

Aidha katika hatua nyingine, Prof. Fortunata Makene amewaasa waandishi wa habari kuzingatia maadili yao ya kazi katika utekelezaji wa majukumu kwani kwa kutofanya hivyo kunaweza kuisababishia jamii hasara kubwa.

Sauti ya Prof Fortunata Songora Makene