Mazingira FM

Uwepo ofisi ya wenye ulemavu Bunda kuwa “mwarobaini”

7 July 2026, 9:00 am

Viongozi wa wenye ulemavu wakijadili changamoto zinazowakabili mbele ya katibu wa mbunge Bunda mjini na mwenyekiti wa UWT Bunda

Kutokuwa na ofisi kunawalazimu watu wenye ulemavu kuzunguka sehemu mbalimbali wanapotafuta msaada

Na Edward Lucas

Viongozi wa watu wenye ulemavu Wilaya ya Bunda wamesema upatikanaji wa ofisi maalumu utarahisisha utoaji wa huduma kwa wanachama wao, ikiwemo kupokea malalamiko ya ukatili, kutoa ushauri na kuwaunganisha waathirika na taasisi zinazoweza kuwasaidia.

Kauli hiyo imetolewa leo Julai 6, 2026, katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa watu wenye ulemavu, wanachama wao, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Bunda pamoja na mwakilishi wa Mbunge wa Bunda Mjini, kwa lengo la kujadili namna ya kupata ofisi inayokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Wilaya ya Bunda, Kigombe Magige Kigombe, amesema kutokuwa na ofisi kunawalazimu watu wenye ulemavu kuzunguka sehemu mbalimbali wanapotafuta msaada, jambo linalochelewesha huduma na wakati mwingine kuwakatisha tamaa kufuatilia haki zao.

Amesema uwepo wa ofisi pia utarahisisha wadau, taasisi na wananchi wanaotaka kushirikiana na watu wenye ulemavu kuwafikia kwa urahisi kupitia uongozi wao.

Sauti ya Kigombe Magige Kigombe

Kigomba ameongeza kuwa hivi karibuni walikabidhi ombi lao kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda la kupatiwa ofisi, lakini jengo waliloelekezwa kulitumia halifai kutokana na kuwa na nyufa, kukosa huduma ya choo na kuwa dogo kiasi cha kutokidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu.

Kwa upande wake, Katibu wa Mbunge wa Bunda Mjini, Mussa Hussein, amesema baada ya kusikiliza maoni ya viongozi hao wamekubaliana kuendelea kutafuta eneo mbadala litakalokuwa salama na linalofaa zaidi kuliko kutumia gharama kubwa kukarabati jengo lililopo.

Sauti ya Mussa Hussein

Naye Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Bunda, Maryciana Sabuni, amesema ataendelea kushirikiana na watu wenye ulemavu katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili, huku akitoa wito kwa viongozi na wananchi kushiriki katika kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata mazingira salama na huduma zinazostahili bila ubaguzi.

Sauti ya Maryciana Sabuni

Mahitaji ya ofisi kwa watu wenye ulemavu yanatajwa kuwa sehemu ya kuimarisha uratibu wa huduma na upatikanaji wa haki, hususan kwa wanawake na watoto wenye ulemavu ambao mara nyingi hukabiliwa na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na ubaguzi. Hatua za kuweka mazingira rafiki ya kuwafikia zinachangia utekelezaji wa jitihada za kuzuia ukatili dhidi ya makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, kama inavyosisitizwa katika Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II).