Mazingira FM

Mbunge Getere aomba changamoto sekondari ya Sanzate zitatuliwe

28 July 2026, 4:55 pm

Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere akizungumza na viongozi wa halmashauri katika ziara yake kuangalia miundombinu ya elimu kata ya Mugeta July 27, 2026

Shule inakabiliwa na upungufu wa majengo manne ya maabara, wataalamu wa maabara, nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi wa kike pamoja na huduma ya maji safi na salama

Na Mariam Mramba

Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere, amemwomba Afisa Elimu Mkoa wa Mara, Dkt. Baganda Pius, kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kutatua changamoto za uhaba wa miundombinu katika Shule ya Sekondari Sanzate, iliyopo Kata ya Mgeta, akisema hali hiyo inaweza kushusha kiwango cha taaluma iwapo haitapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Mbunge Getere ameyasema hayo leo, Julai 27, 2026, katika kikao kilichowakutanisha viongozi wa sekta ya elimu wa wilaya na mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, viongozi wa vijiji na kata pamoja na wananchi wa eneo hilo, kwa lengo la kujadili namna ya kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Sauti ya Boniphace Getere

Akiwasilisha taarifa ya Shule ya Sekondari Sanzate, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Mwinjuma Omari, amesema shule inakabiliwa na upungufu wa majengo manne ya maabara, wataalamu wa maabara, nyumba za walimu, vyoo vya wanafunzi wa kike pamoja na huduma ya maji safi na salama. Ameiomba Serikali kwa kushirikiana na Mbunge wa Jimbo la Bunda kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi.

Sauti ya Mwinjuma Omari

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, George Mbilinyi, amempongeza Mbunge Getere kwa jitihada zake za kutafuta fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo jimboni humo. Pia amewataka walimu kuwashirikisha wenyeviti wa vijiji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo shuleni ili kuongeza uwazi na kuondoa sintofahamu miongoni mwa wananchi.

Sauti ya George Mbilinyi

Naye Afisa Elimu Sekondari Mkoa wa Mara, Dkt. Baganda Pius, amesema elimu ya mtoto haiishii darasani pekee, bali ni muhimu kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kujitegemea kupitia shughuli kama kilimo cha bustani na upandaji miti ili kuwaandaa kwa maisha ya baadaye. Amesema amepokea changamoto zilizowasilishwa na ataendelea kuzifanyia kazi.

Sauti ya Dkt. Baganda Piu

Katika hatua nyingine, viongozi hao walitembelea Shule ya Msingi Sanzate na Shule ya Msingi Rakana, ambapo Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda walikabidhi mifuko 50 ya saruji pamoja na fedha kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Sanzate.