Mazingira FM

Mwanafunzi apoteza maisha baada ya kudaiwa kuchapwa fimbo na walimu 8

20 August 2026, 9:59 am

Adhabu ya kuchapwa fimbo ilitolewa kwa wanafunzi na walimu waliokuwa katika foleni

Na Adelinus Banenwa

Taharuki imetanda katika Shule ya Sekondari Makongoro, Wilaya ya Bunda, baada ya mwanafunzi wa kidato cha sita, Peter Maira (19), anayedaiwa kufariki baada ya kupewa adhabu ya kuchapwa fimbo na walimu kufuatia kufeli mtihani.

Maira, ambaye alikuwa akisoma mchepuo wa PCM (Physics, Chemistry na Mathematics), anadaiwa kupewa adhabu hiyo pamoja na wanafunzi wengine baada ya matokeo ya mtihani.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Makongoro B, Kata ya Nyamuswa, Juma Bugarika Magambo, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, akisema maelezo yaliyotolewa na wanafunzi yanaeleza kuwa adhabu ya kuchapwa fimbo ilitolewa kwa wanafunzi na walimu waliokuwa katika foleni akisisitiza kuwa maelezo hayo yanatokana na taarifa zilizotolewa na wanafunzi waliokuwepo.

Sauti ya Mwenyekiti wa Kijiji cha Makongoro B, Kata ya Nyamuswa, Juma Bugarika Magambo

Diwani wa Kata ya Nyamuswa, Joseph Waryoba Kiaro, amesema kwa sasa hali katika shule hiyo imetulia baada ya viongozi wa ngazi ya wilaya kufika na kuzungumza na wanafunzi pamoja na wananchi.

Tukio hilo lilizua taharuki kubwa shuleni na katika jamii inayozunguka shule hiyo, hali iliyodaiwa kusababisha baadhi ya miundombinu kuharibiwa kabla ya viongozi wa serikali kufika eneo hilo na kutuliza hali.

Miongoni mwa viongozi waliofika shuleni hapo ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda, ambaye alikutana na jamii ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Makongoro pamoja na wananchi katika hatua za kutuliza taharuki iliyojitokeza.

Kiaro amesema tukio hilo lilisababisha hofu na taharuki kubwa, lakini hatua zilizochukuliwa na viongozi zimefanikisha kurejesha utulivu katika eneo hilo.

Amesema kwa sasa suala hilo limeachiwa vyombo vya usalama ambavyo vinaendelea na uchunguzi ili kubaini chanzo halisi cha kifo cha mwanafunzi huyo, pamoja na mazingira yote yaliyozunguka tukio hilo.

Sauti ya Diwani wa Kata ya Nyamuswa, Joseph Waryoba Kiaro

Kifo cha Peter Maira kimeibua maswali kuhusu namna adhabu za kinidhamu zinavyotolewa shuleni, huku majibu ya kina kuhusu chanzo cha kifo chake yakisubiriwa kutoka kwa vyombo vinavyofanya uchunguzi.

Tunaendelea na jitihada za kuwatafuta jeshi la polisi kujua chanzo halisi cha kifo na hasa wahusika ni nani.