Mazingira FM
Mazingira FM
16 September 2026, 9:49 pm

Bima na mbinu bora za usimamizi wa hatari yanaweza kupunguza hasara za kifedha wakati wa majanga, kuongeza uthabiti wa uwekezaji na kusaidia wakulima kuendelea na uzalishaji baada ya kupata fidia
Na Adelinus Banenwa
Wakulima wametakiwa kutumia bima ya mazao kama njia ya kujikinga dhidi ya hasara zinazoweza kusababishwa na majanga ya asili, ikiwemo mafuriko, ukame, upepo mkali, magonjwa na wadudu. Akizungumza kuhusu bima ya mazao na usimamizi wa hatari katika kilimo, Helton Dikson Mtani, Afisa Kilimo kutoka GGF kupitia Mradi wa LCSL, amesema bima ni utaratibu wa kifedha unaomlinda mkulima dhidi ya athari za majanga hayo.
Mtani amesema kuwa kuwa na bima humsaidia mkulima kujilinda dhidi ya hasara za kifedha, kwa kuwa shughuli za kilimo huhitaji gharama kubwa, ikiwemo ununuzi wa mbegu na pembejeo. Amesema fidia inayopatikana baada ya kutokea kwa janga inaweza kumwezesha mkulima kurejea katika uzalishaji, kuongeza uwezo wa kununua pembejeo na kuendelea kuwekeza katika kilimo.
Aidha, amesema bima ya mazao inaweza kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan ukame na mafuriko, pamoja na kuongeza uwezo wa wakulima kupata mikopo kutoka taasisi za kifedha kutokana na kuwa na kinga dhidi ya hasara. Ameongeza kuwa hali hiyo inaweza kuongeza kujiamini kwa wakulima katika kufanya uwekezaji na kuchochea uzalishaji wenye tija.

Katika kusimamia hatari za kilimo, Mtani amewataka wakulima kutumia mbegu zinazostahimili ukame na magonjwa, kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kulima zaidi ya zao moja katika shamba. Pia amesisitiza matumizi ya kilimo hifadhi kwa ajili ya kutunza unyevunyevu na rutuba ya udongo, kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua, kutumia udhibiti shirikishi wa wadudu pamoja na kujiunga na vikundi vya wakulima ili kupata elimu, taarifa za masoko na huduma nyingine muhimu.
Amesema matumizi ya bima na mbinu bora za usimamizi wa hatari yanaweza kupunguza hasara za kifedha wakati wa majanga, kuongeza uthabiti wa uwekezaji na kusaidia wakulima kuendelea na uzalishaji baada ya kupata fidia. Kwa upande mwingine, hatua hizo zinaweza kuchangia kuimarisha usalama wa chakula na lishe pamoja na kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Hata hivyo, Mtani amesema bado kuna changamoto zinazokwamisha matumizi mapana ya bima ya mazao, ikiwemo uelewa mdogo wa wakulima kuhusu huduma hizo, gharama za awali za kujiunga na bima, upatikanaji mdogo wa taasisi na huduma za bima ya mazao, pamoja na muda mrefu unaoweza kutumika katika kufanya tathmini ya hasara. Amesema elimu zaidi inahitajika ili kuwajengea wakulima uelewa kuhusu umuhimu wa bima na namna inavyoweza kuwasaidia kupunguza hatari katika shughuli za kilimo.