Mazingira FM
Mazingira FM
8 September 2026, 10:27 am

Amesema ziara hiyo ni fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao moja kwa moja na viongozi wa serikali, hivyo wananchi wanapaswa kuitumia ipasavyo.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, amewakaribisha wananchi kujitokeza kwa wingi katika ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Nchemba, anayetarajiwa kufanya ziara ya siku mbili wilayani Bunda, Septemba 11 na 12 mwaka huu.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Mhe. Kaminyoge amesema kuwa Septemba 11, Waziri Mkuu atafanya ziara katika Jimbo la Bunda, ambapo atakagua Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na baadaye kufanya mkutano wa hadhara na wananchi katika eneo la Nyamuswa.
Amesema Septemba 12, Waziri Mkuu ataendelea na ziara katika Jimbo la Mwibara, ambako atafanya mkutano na wananchi na kusikiliza kero na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika viwanja vya kibara .
Aidha, Mhe. Kaminyoge ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika mikutano hiyo, huku akiwataka wananchi wenye kero na changamoto mbalimbali kufika na kuzifikisha ili zipatiwe majibu na ufumbuzi.
Mhe. Kaminyoge amesema ziara hiyo ni fursa kwa wananchi kueleza changamoto zao moja kwa moja na viongozi wa serikali, hivyo wananchi wanapaswa kuitumia ipasavyo.