Mazingira FM

Waiomba serikali kusafisha mazingira baada ya kifo cha mtoto

7 July 2026, 10:17 am

Moja ya wakazi wa Nyasura Bunda akizungumzia kadhia ya uhalifu kwenye maeneo yasiyoendelezwa

Wananchi wameiomba serikali kuanzia ngazi ya mtaa hadi wilaya kuziagiza taasisi zinazomiliki maeneo ambayo hayajaendelezwa kuyafanyia usafi au kuyatoa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo, wakisema maeneo hayo yamekuwa maficho ya wahalifu.

Na Adelinus Banenwa

Wananchi wa Kata ya Nyasura, Wilaya ya Bunda, wameiomba serikali kuanzia ngazi ya mtaa hadi wilaya kuziagiza taasisi zinazomiliki maeneo ambayo hayajaendelezwa kuyafanyia usafi au kuyatoa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo, wakisema maeneo hayo yamekuwa maficho ya wahalifu.

Wito huo umetolewa kufuatia tukio la kusikitisha la mtoto Saimoni Juma Bango, ambaye alitoweka Juni 24 kabla ya mwili wake kupatikana Juni 26 ukiwa umetupwa vichakani katika pori la Chuo cha Ualimu Bunda, ukiwa tayari umeharibika.

Wakizungumza wakati wananchi walipojitokeza kufyeka msitu wa eneo hilo, wenyeviti wa mitaa ya Zanzibar, Nyasura B na Makumbusho, yote ya Kata ya Nyasura, waliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi shirikishi kwa kutoa taarifa za wahalifu na kushiriki doria za ulinzi ili kuimarisha usalama wa maeneo yao.

Viongozi hao pia waliwasisitiza wazazi na walezi kuwa walinzi wa kwanza wa watoto wao huku wakiwataka kuacha tabia ya kuwafanyisha watoto shughuli za biashara zinazoweza kuwaweka kwenye mazingira hatarishi.

Polisi wa Kata ya Nyasura, Sajenti Joseph

Kwa upande wake, Polisi wa Kata ya Nyasura, Sajenti Joseph, amesema ulinzi shirikishi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Amesema maeneo yenye misitu au ambayo hayajaendelezwa yanapaswa kufyekwa au kugawiwa kwa wananchi wayatumie kwa shughuli za kilimo ili kuondoa maficho ya wahalifu.

Diwani wa Kata ya Nyasura, Magigi Samwel Kiboko

Naye Diwani wa Kata ya Nyasura, Magigi Samwel Kiboko, amesema tukio la kifo cha mtoto huyo katika mazingira ya kutatanisha halikubaliki na kwamba ni wajibu wa wazazi na jamii kwa ujumla kuhakikisha watoto wanalindwa.

Diwani huyo ameahidi kufuatilia taasisi zote zenye maeneo ambayo hayajaendelezwa ili kuhakikisha yanafanyiwa usafi au yanatolewa kwa wananchi kwa matumizi ya kilimo, hatua ambayo alisema itasaidia kuimarisha usalama.