Mazingira FM

DC Bunda awataka vijana kutumia fursa za mikopo kujikwamua kiuchumi

7 August 2026, 9:22 pm

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge

Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi, hivyo vijana wanapaswa kuzitambua, kuzitumia kwa usahihi na kuanzisha shughuli zitakazowawezesha kuongeza kipato

Na Adelinus Banenwa

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, amewataka vijana kutumia fursa za mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri pamoja na mfuko wa kuwawezesha vijana kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, ili kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Mhe. Kaminyoge ametoa wito huo leo, Agosti 7, 2026, wakati akifungua Kongamano la Vijana Platform kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, lililofanyika katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mara Girls.

Amesema serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa vijana kupitia fursa mbalimbali za kiuchumi, hivyo vijana wanapaswa kuzitambua, kuzitumia kwa usahihi na kuanzisha shughuli zitakazowawezesha kuongeza kipato.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge

Kwa upande wake, Kolman, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambaye pia ni Mratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Halmashauri hiyo, amesema kongamano hilo linalenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu uzalendo na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao.

Baadhi ya vijana walioshiriki kongamano hilo

Amesema fursa hizo zinapatikana katika sekta mbalimbali ikiwemo kilimo, mifugo, uvuvi, biashara, ujasiriamali na ubunifu, huku akieleza kuwa kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa kampeni za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2026.

Ameongeza kuwa, pamoja na kutoa elimu kwa vijana, kongamano hilo pia linahusisha mchakato wa kuchagua uongozi wa vijana ambao utakuwa kiungo kati ya serikali na vijana katika kuwasilisha changamoto, mahitaji na fursa zinazowahusu.

Sauti ya Kolman, Afisa Vijana wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda

Kwa upande wao, baadhi ya vijana walioshiriki kongamano hilo wamesema elimu waliyopata imekuwa na manufaa makubwa, kwa kuwa imewafumbua macho kuhusu namna ya kutambua na kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana katika maeneo yao.

Moja ya watoa mada kwenye kongamano Dr Masinde Bwire

Wamesema baadhi ya fursa hizo ni pamoja na kilimo, uvuvi, biashara na ufugaji, huku wakiiomba serikali kuendelea kutoa elimu na kuwawezesha vijana ili waweze kutumia fursa hizo kujenga maisha yao na kuondokana na utegemezi.

Sauti za baadhi ya vijana walioshiriki kongamano