Mazingira FM

Polisi Jamii waweka mkazo kwenye huduma kwa mteja

11 June 2026, 4:15 pm

Jonas Kaijage, msaidizi wa Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Bunda

Kaijage amesema maboresho hayo yamechangia kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuwezesha kupatikana kwa taarifa nyingi zaidi za uhalifu kutoka katika jamii.

Na Adelinus Banenwa

Jeshi la Polisi linaendelea kuhimiza utoaji wa huduma bora kwa wateja katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano kati ya polisi na wananchi pamoja na kuongeza ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu.

Jonas Kaijage, msaidizi wa Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Bunda, amesema jeshi hilo linaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya kimfumo, ikiwemo matumizi ya lugha rafiki kwa wananchi wanaofika vituoni kutoa taarifa za uhalifu, wahalifu na watuhumiwa.

Akizungumza kupitia Radio Mazingira FM katika mwendelezo wa utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu ulinzi shirikishi na Polisi Jamii, Kaijage amesema maboresho hayo yamechangia kuongeza imani ya wananchi kwa Jeshi la Polisi na kuwezesha kupatikana kwa taarifa nyingi zaidi za uhalifu kutoka katika jamii.

Amesema falsafa ya ulinzi shirikishi na Polisi Jamii, hususan katika eneo la huduma kwa mteja, imeendelea kuimarishwa na kwa sasa imeingizwa katika mtaala wa mafunzo kwa askari polisi.

Kaijage amebainisha kuwa hapo awali kulikuwa na malalamiko kuhusu matumizi ya lugha kali kwa baadhi ya wananchi waliokuwa wakifika vituoni, hali iliyokuwa ikiwafanya waogope au kusita kutoa taarifa za matukio ya kihalifu.

Hata hivyo, amesema hali hiyo imeendelea kupungua kutokana na elimu inayotolewa kwa askari kuhusu umuhimu wa kuwapokea wananchi kwa heshima, kuwasikiliza na kuzungumza nao kwa weledi wakati wa kutoa huduma.

Amesisitiza kuwa kuimarika kwa huduma kwa wateja ndani ya Jeshi la Polisi ni sehemu ya juhudi za kujenga imani kwa wananchi na kuifanya jamii kuwa mshirika muhimu katika kudumisha amani, usalama na utulivu.

Sauti ya Jonas Kaijage, msaidizi wa Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Bunda