Mazingira FM

Bei ya pamba msimu wa 2025/2026 kujulikana May 2 Bariadi

1 May 2025, 8:24 pm

Macho na masikio ya wakulima wengi wa zao hilo nchini yatakuwa katika hafla hiyo, kwani matamanio ya wengi ni kuona bei ambayo itatangazwa

Na Adelinus Banenwa

Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) inatarajia kutangaza bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo msimu wa 2025/2026 May 2, 2025.

Hafla ya kutangaza bei inatarajiwa kufanyika katika mtaa wa Mwakibuga uliopo kwenye Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu.

Macho na masikio ya wakulima wengi wa zao hilo nchini yatakuwa katika hafla hiyo, kwani matamanio ya wengi ni kuona bei ambayo itatangazwa inaweza kufikia Sh 2,000 kwa kilo moja.

Ikumbukwe kuwa bei elekezi ya ununuzi wa zao hilo ambayo ilitangazwa na bodi msimu wa 2024/2025 ilikuwa Sh 1,150 kwa kilo moja ya pamba daraja la kwanza na daraja la pili ikiwa ni Sh 575 kwa kilo moja.

Katika hatua nyingine pia wakulima wanasubiri kujua mfumo utakaotumika wa ununuzi wa zao la pamba kwa msimu huu ama ni wa AMCOS au wa makampuni yenyewe kuweka mawakala.

Akizungumza kupitia kipindi cha Asubuhi leo kinachorushwa na radio Mazingira Fm katibu wa AMCOS Kunzugu ndugu Nyang’era Lukiko amesema endapo ikiamuliwa mfumo wa AMCOS kuendelea, udhibiti wa pamba safi utakuwepo ila ikitokea ukatumika mfumo wa makampuni kuweka mawakala wao huwenda ikashuhudiwa pamba yenye maji hali itakayopelekea pamba kushuka katika soko la kimataifa.

katibu wa AMCOS Kunzugu Nyang’era Lukiko