Mazingira FM

Mwenge wa uhuru wakagua miradi saba ya yaendeleo Bunda

1 August 2026, 7:46 pm

Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuendelea na mbio zake katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara kwa lengo la kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo, sambamba na kuhamasisha uzalendo, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.

Na Adelinus Banenwa

Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 leo umeingia rasmi mkoani Mara ukianzia Halmashauri ya Mji wa Bunda, ambapo umekimbizwa umbali wa kilometa 70 na kutembelea miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.4.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mheshimiwa Aswege Enock Kaminyoge, miradi iliyotembelewa ni pamoja na ukumbi wa mwekezaji wenye thamani ya shilingi milioni 600, mradi wa maji wa Ruwasa Chang’uge wenye thamani ya shilingi milioni 150, ujenzi wa ofisi ya Mtaa wa Bitaraguru wenye thamani ya shilingi milioni 30, ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Manyamanyama, nyumba za watumishi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Bunda pamoja na mradi wa kikundi cha vijana uliopo katika Kata ya Bunda Stoo.

Sauti ya Aswege Enock Kaminyoge

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa miradi hiyo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda, ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kusimamia na kutekeleza miradi hiyo kwa kuzingatia taratibu, ubora na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Michael Mwang’onda akisalimiana na mkuu wa wilaya ya Bunda Aswege Enock Kaminyoge

Aidha, Mwang’onda amewahimiza wananchi wa Bunda na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuendelea kudumisha amani, umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo endelevu na utekelezaji wa miradi yenye manufaa kwa jamii.

Sauti ya Wazo Michael Mwang’onda

Mwenge wa Uhuru unatarajiwa kuendelea na mbio zake katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mara kwa lengo la kukagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi katika miradi ya maendeleo, sambamba na kuhamasisha uzalendo, uwajibikaji na ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo.