Mazingira FM

Akutwa amefariki katika mazingira ya kutatanisha mwili watelekezwa porini

26 June 2026, 11:32 pm

Waombolezaji wakiendelea na shughuli za mazishi ya mtoto aliyekutwa amefariki na mwili kutelekezwa porini

Mtoto huyo alipotea nyumbani tangu Juni 24, 2026, baada ya kwenda na wenzake kuuza maandazi katika eneo la Stendi ya Nyasura.

Na Adelinus Banenwa

Mtoto aliyetambulika kwa jina la Saimoni Juma Bango (11), mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Mazoezi na mkazi wa Kata ya Nyasura, amekutwa amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha katika eneo la Chuo cha Ualimu Bunda.

Akizungumza na Radio Mazingira FM, mama mkubwa wa marehemu, Censilia Elenest Masige, amesema mtoto huyo alipotea nyumbani tangu Juni 24, 2026, baada ya kwenda na wenzake kuuza maandazi katika eneo la Stendi ya Nyasura.

Censilia amesema Saimoni hakurejea nyumbani siku hiyo, hali iliyowalazimu kuanza kumtafuta. Leo walipokea taarifa za kuonekana kwa mbwa akiwa amebeba kiungo kinachodhaniwa kuwa cha binadamu, ambacho walikitambua kuwa ni cha mtoto huyo. Baadaye, walielekezwa mahali ulipokuwa mwili wake, ambao ulikuwa umeharibika.

waombolezaji wakiendelea na shughuli za mazishi ya mtoto aliyekutwa amefariki na mwili kutelekezwa porini
Sauti ya mama mkubwa wa marehemu, Censilia Elenest Masige

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Zanzibar, Nyabaturi Ogora, amesema alipokea taarifa za kupotea kwa mtoto huyo tangu Juni 24 na kuwashauri wazazi wake kutoa taarifa katika kituo cha polisi ili kuanza uchunguzi.

Nyabaturi amesema leo, Juni 26, alipata taarifa za kuonekana kwa kiungo cha binadamu kikiwa kimebebwa na mbwa katika eneo la Chuo cha Ualimu Bunda. Alifika eneo la tukio na baada ya kujiridhisha kuwa ni kiungo cha binadamu, aliwajulisha wazazi wa mtoto pamoja na viongozi wengine na Jeshi la Polisi, ambao walifika kwa ajili ya uchunguzi na hatua nyingine za kisheria.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Zanzibar, Nyabaturi Ogora
Sauti Mwenyekiti wa Mtaa wa Zanzibar, Nyabaturi Ogora

Aidha, Nyabaturi ametoa wito kwa wazazi na walezi kuongeza uangalizi kwa watoto wao, akieleza kuwa matukio ya uhalifu yanayoendelea kwa sasa yanahatarisha usalama wa watoto, hivyo ni muhimu kuchukua tahadhari ili kulinda maisha yao.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho na kuwabaini waliohusika na tukio hilo.