Mazingira FM
Mazingira FM
17 November 2026, 4:15 pm

Madai ya mahari au fidia pindi wazazi wanapojitokeza inayochangia kuongezeka kwa vitendo vya utelekezaji wa watoto na kuwanyima haki ya kupata malezi kutoka kwa wazazi wao.
.Na Edward Lucas.
Bibi na babu wametakiwa kuacha tabia ya kuwazuia wazazi kuwachukua watoto wao kwa madai ya mahari au fidia, hatua inayochangia kuongezeka kwa vitendo vya utelekezaji wa watoto na kuwanyima haki ya kupata malezi kutoka kwa wazazi wao.
Wito huo umetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Warioba Juma Warioba, wakati akizungumza na Radio Mazingira FM katika kipindi cha ASUBUHI LEO, alipokuwa akielezea changamoto ya utelekezaji wa watoto.
Warioba amesema baadhi ya wazazi wamekuwa na tabia ya kuwaachia watoto wao kwa ndugu, marafiki au wazazi wao, bila kuhakikisha wanapata matunzo na mahitaji muhimu ya kijamii.
Akifafanua zaidi, amesema baadhi ya mababu na mabibi wamekuwa wakiwazuia wazazi kuwachukua watoto wao wanapojitokeza kufanya hivyo, kwa madai ya kulipwa fidia au mahari, hali inayowafanya baadhi ya wazazi kushindwa kutimiza masharti hayo na kuacha watoto wakiendelea kulelewa na ndugu zao bila uhakika wa huduma muhimu.
Ameeleza kuwa watoto wanaokosa malezi na uangalizi wa kutosha wako katika hatari ya kukumbwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo kuingia katika mahusiano ya kimapenzi wakiwa na umri mdogo, utoro shuleni, mimba na ndoa za utotoni, pamoja na kutelekezwa wanapopata ujauzito au kujifungua.