Mazingira FM
Mazingira FM
20 October 2026, 1:19 pm

Aidha, elimu ya mazingira inawajengea wananchi uelewa kuhusu umuhimu wa misitu katika kufyonza hewa ukaa, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda bioanuwai.
Na Adelinus Banenwa
Elimu ya mazingira ina nafasi muhimu katika kuwasaidia wananchi kuelewa athari za mabadiliko ya tabianchi na kuchukua hatua za kukabiliana nazo. Haya yamebainika baada ya kutembelea Kata ya Kamgegi, iliyopo Wilaya ya Butiama, katika utekelezaji wa mradi wa LCSL chini ya Shirika la GGF, ambapo wananchi wanajishughulisha na ufugaji wa nyuki kwa lengo la kulinda misitu asilia na kuhifadhi mazingira. Kupitia shughuli hii, wananchi wanapata kipato kutokana na uzalishaji wa asali huku wakihamasika kutunza misitu ambayo ni muhimu katika kudhibiti mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, elimu ya mazingira inawajengea wananchi uelewa kuhusu umuhimu wa misitu katika kufyonza hewa ukaa, kuhifadhi vyanzo vya maji, kuzuia mmomonyoko wa udongo na kulinda bioanuwai. Mfano wa wananchi wa Kata ya Kamgegi unaonesha jinsi ufugaji wa nyuki unavyoweza kuunganisha uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kiuchumi, hivyo kuimarisha ushiriki wa jamii katika kulinda rasilimali za asili na kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.