Mazingira FM
Mazingira FM
14 October 2026, 9:50 pm

Baadhi ya wananchi wamesema kutembelea Makumbusho ya Mwalimu Nyerere kunawapa nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu historia ya maisha ya hayati Mwalimu Nyerere na mchango wake katika ujenzi wa taifa.
Na Edward Lucas.
Makumbusho ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yaliyopo wilayani Butiama mkoani Mara yanaendelea kuwa sehemu muhimu ya kujifunza historia ya taifa kwa vitendo, huku wanafunzi na wananchi wanaotembelea eneo hilo wakipata fursa ya kufahamu zaidi maisha na uongozi wa Baba wa Taifa.
Wakizungumza katika viwanja vya makumbusho hayo, baadhi ya wananchi wamesema kutembelea eneo hilo kunawapa nafasi ya kujifunza mambo mbalimbali kuhusu historia ya maisha ya hayati Mwalimu Nyerere na mchango wake katika ujenzi wa taifa.
Kwa upande wao, baadhi ya wanafunzi waliotembelea makumbusho hayo wamesema kujifunza kwa vitendo kunawasaidia kuelewa historia kwa undani zaidi, tofauti na kutegemea masomo ya nadharia pekee darasani.

Akizungumzia umuhimu wa makumbusho hayo katika kipindi hiki cha maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere, Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Mwalimu Nyerere wilayani Butiama, Paul Kado, amesema wameendelea kupokea wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujifunza historia ya kiongozi huyo na kuenzi kazi mbalimbali alizozifanya.

Makumbusho ya Mwalimu Nyerere yaliyopo Mwitongo, Butiama, yanahifadhi kumbukumbu na vielelezo vinavyoelezea maisha ya Baba wa Taifa, mchango wake katika kupigania uhuru wa Tanganyika na uongozi wake baada ya uhuru.
Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifariki dunia tarehe 14 Oktoba 1999 akiwa na umri wa miaka 77 katika Hospitali ya St. Thomas jijini London, Uingereza, baada ya kuugua saratani ya damu. Kila mwaka, tarehe hiyo hutumika kumkumbuka na kuenzi mchango wake katika historia ya Tanzania.