Mazingira FM
Mazingira FM
9 October 2026, 1:49 pm

Kupitia risala hiyo, wanafunzi wameiomba Serikali kuwajengea mabweni ili kuwawezesha wanafunzi wanaotoka mbali kupata mazingira bora ya kujifunzia
Na Juma Hangi
Ukosefu wa mabweni kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali, pamoja na uhaba wa vifaa vya TEHAMA na michezo, ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili Sekondari ya Guta wilayani Bunda.
Changamoto hizo zimetajwa katika risala ya wanafunzi wa Kidato cha Nne wakati wa mahafali yaliyofanyika leo shuleni hapo, ambapo wahitimu 136, wavulana 80 na wasichana 56, wanatarajiwa kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari.
Kupitia risala hiyo, wanafunzi wameiomba Serikali kuwajengea mabweni ili kuwawezesha wanafunzi wanaotoka mbali kupata mazingira bora ya kujifunzia, pamoja na kusaidia upatikanaji wa vifaa vya michezo na TEHAMA.

Mkuu wa shule, Petro Sadala, amesema licha ya kuwa na walimu watatu waliobobea katika TEHAMA, shule hiyo haina vifaa vya kutosha, hivyo ameomba msaada wa kompyuta 20 na projector moja ili kuongeza ujuzi wa wanafunzi.

Akijibu maombi hayo, Katibu Mwenezi wa CCM Wilaya ya Bunda, Gasper Charles Petro, aliyemwakilisha Mbunge wa Bunda Mjini Ester Amos Bulaya, amesema mbunge huyo atatoa printer mashine moja yenye thamani ya Sh milioni 3 kwa ajili ya kusaidia kuboresha ujifunzaji na kuinua ufaulu shuleni hapo.