Mazingira FM
Mazingira FM
7 October 2026, 6:41 pm

Mbunge ameahidi kutoa shilingi milioni nane katika awamu ya kwanza kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jiko la kisasa
Na Juma Hangi
Ujenzi wa jiko la kisasa ni miongoni mwa mahitaji makubwa yanayoikabili Shule ya Sekondari Sazira iliyopo Kata ya Sazira, Wilaya ya Bunda, huku wanafunzi wakiomba Serikali kusaidia upatikanaji wa jiko hilo.
Wamesema ujenzi wa jiko bora utasaidia kurahisisha kazi ya wapishi, kuimarisha afya na usalama wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya shule.
Aidha wanafunzi hao pia wameomba kuongezwa kwa mabweni kwa wanafunzi wanaotoka maeneo ya mbali pamoja na kujengwa kwa nyumba zaidi za walimu.

Hayo yamesemwa Oktoba 7, 2026, katika risala ya wanafunzi wa Kidato cha Nne wakati wa Mahafali ya 19 ya shule hiyo. Jumla ya wanafunzi 177, wakiwemo wavulana 100 na wasichana 77, wanatarajia kufanya mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari.
Mkuu wa Shule ya Sekondari Sazira, Edga Sibola, amesema shule hiyo bado inakabiliwa na ukosefu wa mabweni , mfumo wa umeme katika baadhi ya vyumba vya madarasa pamoja na jiko la kupikia.

Ameiomba Serikali na wadau kuendelea kushirikiana na shule hiyo kutatua changamoto hizo, huku akiishukuru Serikali na Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Amos Bulaya, kwa mchango wao katika maendeleo ya shule.
Akijibu risala hiyo, mwakilishi wa Mbunge wa Bunda Mjini, Gasper Petro Charles, amesema mbunge ameahidi kutoa shilingi milioni nane katika awamu ya kwanza kwa ajili ya kuanza ujenzi wa jiko la kisasa, huku awamu ya pili ikiwa ni shilingi milioni nane, hivyo kufikisha jumla ya shilingi milioni 16.
Gasper pia amewataka wahitimu wa Kidato cha Nne kuwa raia wema baada ya kumaliza mitihani yao.