Mazingira FM

Wazazi waonywa kusambaza picha za watoto hovyo

14 November 2026, 8:21 pm

Wakili Aloyce Kajitanus katika kipindi cha ufahamu wa sheria radio Mazingira FM

Wakili Kajitanus ametoa tahadhari kwa wananchi wanaopiga na kusambaza picha za watu waliojeruhiwa au waliofariki katika maeneo ya ajali.

Na Adelinus Banenwa

Wananchi wametahadharishwa dhidi ya tabia ya kupiga na kusambaza picha za utupu, picha za kingono pamoja na picha za watoto katika mazingira yanayokiuka haki na utu wao, wakielezwa kuwa vitendo hivyo vinaweza kuwa kosa la jinai na kusababisha adhabu kali kwa mujibu wa sheria za Tanzania.

Akizungumzia suala hilo, Wakili Aloyce Kajitanus amesema Sheria ya Makosa ya Kimtandao ya mwaka 2015, kupitia kifungu cha 14, inakataza kusambaza maudhui ya ponografia kwa njia ya mifumo ya kompyuta, ambapo mtuhumiwa anaweza kukabiliwa na faini isiyopungua shilingi milioni 20 au kifungo kisichopungua miaka saba, au vyote kwa pamoja.

Amesema Ibara ya 16 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inalinda haki ya faragha ya mtu, familia na mawasiliano yake binafsi, huku Sheria ya Mtoto ikimtambua mtoto kuwa ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18.

Aidha, ameeleza kuwa kifungu cha 159(1) cha Sheria ya Mtoto kinaweka masharti kuhusu uchapishaji wa picha na taarifa zinazohusu watoto, akisisitiza kuwa mzazi, ndugu au jirani anaweza kuwajibika kisheria endapo atapiga na kusambaza picha za mtoto katika mazingira ya kingono. Hata hivyo, sheria haizuii wazazi kushiriki picha za kawaida za watoto wao katika matukio kama sherehe za siku za kuzaliwa.

Katika hatua nyingine, Wakili Kajitanus ametoa tahadhari kwa wananchi wanaopiga na kusambaza picha za watu waliojeruhiwa au waliofariki katika maeneo ya ajali, akiwataka kuheshimu utu na faragha ya waathirika pamoja na familia zao, na kuepuka kusambaza maudhui yanayoweza kukiuka sheria.

Sauti ya wakili Aloyce Kajitanus